Simba yatinga makundi Kombe la Shirikisho Afrika

Sunday December 05 2021
SIMBA MAKUNDI PIC
By Daudi Elibahati

KLABU ya Simba imefanikiwa kuingia hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika licha ya kufungwa mabao 2-1 na Red Arrows katika Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Zambia.

Mchezo huu wa pili wa marudiano ulishuhudia Red Arrows ikipata bao la kwanza kupitia kwa Ricky Banda dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza kwa shuti kali la mguu wa kushoto lililomshinda golikipa wa Simba, Aishi Manula.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa wenyeji kulishambulia lango la Simba ambapo dakika 47, Saddam Phiri aliipatia Red Arrows bao la pili kwa kichwa safi baada ya uzembe uliofanywa na idara ya ulinzi wa kati ya Simba iliyokuwa ikiongozwa na Pascal Wawa na Henock Inonga.

Simba walipata bao la kufutia machozi dakika ya 67 kupitia kwa kiungo Hassan Dilunga aliyepiga shuti kali lililomshinda kipa wa Red Arrows Charles Kalumba.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufuzu hatua hiyo baada ya ushindi wa jumla wa mabao 4-2, baada ya awali kushinda mabao 3-0, Novemba 28 katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

Advertisement