Simba yatimkia Zanzibar kuiwinda Yanga

Muktasari:

  • Simba itakuwa ugenini ikiivaa Yanga ambayo inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mabao 5-1 mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Kikosi cha Simba, chini ya Kocha Abdelhak Benchikha kinatarajia kuondoka kesho asubuhi kwenda Zanzibar kwa ajili ya kambi ya siku tatu kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya watani wao wa jadi Yanga, utakaopigwa Jumamosi ijayo.

Simba itakuwa ugenini ikiivaa Yanga ambayo inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mabao 5-1 mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa wachezaji wote wakiongozwa na kocha mkuu wataondoka kesho saa 4:00 asubuhi kwa ajili ya kambi hiyo ya siku tatu na watarudi Dar es Salaam Ijumaa asubuhi.

“Timu itaondoka kesho asubuhi na itarudi Ijumaa tayari kwa ajili ya kuivaa Yanga Jumamosi, tunakwenda Zanzibar kwa sababu kocha ametaka iwe hivyo, wachezaji wote tunatarajia kuondoka nao.” kimesema chanzo hicho.

Kwenda kwa Simba Kisiwani Zanzibar itakuwa ni mara ya pili kwa siku za hivi karibuni baada ya awali kufanya hivyo wakijiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali dhidi ya Al Ahly na baada ya kurejea walikubali kichapo cha bao 1-0.