Simba yatafuna kiporo, Sarr aibeba

Muktasari:
- Timu hiyo ilitoka na kicheko hapo jana kwa bao la kiungo, Babacar Sarr kutoka Senegal aliyesajiliwa dirisha dogo, ambalo alilifunga kwa kichwa dakika ya 82 akimalizia krosi nzuri ya kupande wa kushoto kutoka kwa Kibu Denis.
Simba imemaliza kibabe viporo vyake vya Kanda ya Ziwa kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold, ukiwa ni wa tatu katika mechi nne huku ikiambulia sare moja dhidi ya Azam FC Ijumaa iliyopita.
Timu hiyo ilitoka na kicheko hapo jana kwa bao la kiungo, Babacar Sarr kutoka Senegal aliyesajiliwa dirisha dogo, ambalo alilifunga kwa kichwa dakika ya 82 akimalizia krosi nzuri ya kupande wa kushoto kutoka kwa Kibu Denis.
Katika michezo minne ya Kanda ya Ziwa, Simba imepata haijaruhusu bao katika michezo mitatu, ikishinda mitatu dhidi ya Mashujaa FC, Tabora United na Geita Gold na kupata sare mbele ya Azam FC.

Sarr alifunga bao hilo ambalo ni la kwanza kwake tangu atue Simba, dakika 12 tu tangu alipoingia dakika ya 70 kuchukua nafasi ya Sadio Kanoute, na kuinusuru Simba ambayo mambo yalikuwa yameshakuwa magumu ikielekea kupata sare ya pili mfululizo kwenye Uwanja huo.
Matokeo hayo yanawafanya Simba kupata ushindi wa 10 msimu huu kwenye ligi na kufikisha pointi 33 kwenye msimamo ikiishusha Azam na kukamata nafasi ya pili, huku Yanga ikiendelea kukaa kileleni na pointi 40, Azam ikiwa ya tatu na alama 32.

Ushindi huo pia unaendeleza rekodi dhidi ya Wachimba Dhahabu ambao hawajapata ushindi kwenye michezo mitano sasa dhidi ya Simba wakiambulia sare moja na kufungwa nne.
Kichapo hicho kwa Geita Gold kinakuwa cha kwanza Ligi Kuu na kwenye mashindano yote tangu akabidhiwe majukumu kocha Denis Kitambi aliyetokea Ihefu, akichukua nafasi ya Hemed Suleiman 'Morocco' aliyefungashiwa virago Desemba 20, mwaka jana.
Katika mchezo huo ambao umepigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Simba ilionyesha kiwango bora huku mastaa wake Clatous Chama, Pa Jobe na Kibu Denis wakionekana kuelewana zaidi na kuwasumbua mabeki wa wa pembeni wa Geita Gold.
DAKIKA 45 ZA CHAMA
Chama amepiga kona sita, faulo mbili, huku Saido akipiga kona tano na faulo moja.
Mchezo huo haukuwa na kasi kubwa licha ya Simba kutawala zaidi kwa dakika 45, lakini Geita Gold walisimama imara wakicheza wengi kwenye eneo lao na kuwapa wakati mgumu Simba kupenya na kuleta madhara.
Wachimba Dhahabu hao walifanya shambulizi moja pekee kipindi cha kwanza kumjaribu kipa Aishi Manula kupitia shuti la Jonathan Ulaya katika dakika ya 45, likiwa ni shuti lao pekee lililolenga lango.
Katika dakika 45, Simba ilifanya mashambulizi sita ambayo yalizaa kona sita, lakini zote hazikuwapa faida hivyo kulazimishwa kwenda mapumziko bila kufungana.
Dakika 45 za kwanza zilikuwa za Mwamba wa Lusaka, Chama ambaye mipira yote ya kutengwa ya Simba ameipiga yeye, ambapo alipiga mipira ya kona sita na miwili ya faulo, huku kipindi cha pili akipiga faulo moja pekee ambayo alianzishiana na Saido Ntibazonkiza kabla ya kutolewa na kumpisha Luis Miquissone.
Katika dakika ya 21, mchezaji wa Geita Gold alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea vibaya beki wa Simba, Che Malone ikiwa ni ekee ambayo ilitolewa na mwamuzi katika kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko ya wachezaji dakika ya 46 Simba ikimpumzisha Mzamiru Yassin na kuingia Saido Ntibazonkiza, huku Geita Gold akitolewa Mahamud na Edmund John na kuingia Tariq Seif na Nassoro Hamdun.
Baada ya kuingia dakika ya 46, mipira ya kutengwa ya Simba ilihamia kwa Ntibazonkiza ambaye alianza kupiga kona za timu hiyo. Alipiga kona tano na faulo moja.
Dakika ya 70, Simba ilifanya mabadiliko mengine ya wachezaji ikiwapumzisha Chama, Sadio Kanoute na Pa Jobe na kuingia Miquissone, Sarr na Fredy Michael, huku Geita ikimtoa Jonathan Ulaya na kuingia Erick Mwijage.
Dakika ya 75, Kenedy Juma wa Simba alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Hamdun ikiwa ni ya pili ya njano kwenye mchezo huo ikitangulia na ile ya dakika ya 21 aliyoipata beki wa Geita, Ulaya.
KIRUMBA KUGUMU KWA GEITA
Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambao Geita Gold imekuwa ikiutumia kwa mechi zake za Ligi Kuu dhidi ya Simba na Yanga umeendelea kuwa mgumu kwao kwani katika mechi saba ilizocheza haijapata ushindi.
Tangu msimu wa 2021/2022 timu hiyo imekutana na Simba mara mbili ikipoteza moja na sare moja na ilikutana na Yanga mara tatu na kupoteza zote, huku ikitoka sare mbili dhidi ya Azam na Singida Fountain Gate
BENCHIKA BADO HATABIRIKI
Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchika ameendelea kutotabirika kwenye vikosi anavyoanga kila mechi baada ya kufanya mabadiliko ya wachezaji kuanzia watatu mpaka wanne kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa, Tabora United na Azam FC.
Jana alifanya hivyo akiwaanzisha Mzamiru Yassin, Pa Jobe, Sadio Kanoute, Kenedy Juma, Shomari Kapombe na Aishi Manula wakichukua nafasi ya Israel Mwenda, Hussein Kazi, Ayoub Lakred, Fredy Michael na Saido Ntibazonkiza