Simba yapiga bao vigogo 8 Afrika

Muktasari:

Droo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa kuchezeshwa Aprili 30 mwaka huu ambapo timu nne zilizoongoza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu hii zitakutanishwa na timu nne zilizoshika nafasi ya pili.

Wakati Simba ikijihakikishia kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimum huu pamoja na uongozi wa kundi A, hali ni tete kwa timu nane zenye historia kubwa barani humu ambazo hadi sasa hazijawa na uhakika wa kusonga mbele kwenye makundi yao huku nyingine zikiwa zimeshaaga mashindano hayo.

Ushindi wa mabao 4-1 nyumbani dhidi ya AS Vita Club ya DR Congo jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliifanya Simba iwe na uhakika wa kuongoza kundi A baada ya kufikisha pointi 13 huku ukiipa tiketi ya kucheza robo fainali.

Lakini wakati Simba ikifanya hivyo, timu nane vigogo zimepigwa bao na Simba sio tu kwa kuongoza kundi, bali pia kufuzu robo fainali ambapo nyingi zinasubiria mechi za mwisho kujua hatima zao na nyingine zimeshaaga mashindano hayo.

Washindi wa taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 1973, AS Vita Club yenyewe imeachwa kwenye mataa kwani imeaga mashindano hayo katika kundi A kufuatia kichapo cha mabao 4-1 ilichokipata jana kutoka kwa Simba ikiungana na Al Merrikh iliyowahi kufika nusu fainali mwaka 2015 na hivyo kuziacha Simba na Al Ahly kusonga mbele.

Al Hilal ya Sudan iliyowahi kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1987, hadi sasa hawajawa na uhakika wa kutinga robo fainali kupitia kundi B kwani wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi nne na wanahitajika kupata ushindi katika mechi yao ya mwisho ugenini dhidi ya TP Mazembe huku wakiombea CR Belouizdad wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi sita, wapoteze au watoke sare ugenini na Mamelodi Sundowns ili wao wasonge mbele.

Mamelodi Sundowns inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi 13, tayari imeshafuzu kwani pointi zake haziwezi kufikiwa na timu nyingine.

Mshtuko mkubwa katika kundi hilo na mashindano hayo kiujumla msimu huu ni kutolewa mapema kwa mabingwa mara tano wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe ambayo baada ya kichapo cha mabao 2-0 ugenini kwa CR Belouizdad juzi, wameaga rasmi mashindano hayo kwani wamebaki wanashika mkia wakiwa na pointi mbili ambazo hazitoshi kuwafanya wafikie zile za timu mbili za juu kwenye kundi hilo hata wakipata ushindi katika mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya Al Hilal.

Mabingwa wa Kombe la Washindi Afrika, mwaka 1978, Horoya ya Guinea bado haijafuzu robo fainali licha ya kushika nafasi ya pili kwenye kundi C wakiwa na pointi nane, na wanahitaji ushindi au sare tasa katika mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya Kaizer Chiefs ili wasonge mbele.

Kaizer Chiefs iliyowahi kutwaa Kombe la Washindi Afrika mwaka 2001, ni kigogo kingine ambacho bado hakijajihakikishia tiketi ya robo fainali licha kukusanya pointi nane katika kundi hilo C, na wanahitaji ushindi au sare ya mabao ugenini dhidi ya Horoya katika mechi ya mwisho waweze kutinga robo fainali wakati Wydad Casablanca wenye pointi 10 wakiwa wamefuzu huku Petro Luanda waliowahi kufika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1997 wakiwa wameshaaga na pointi yao moja.

Vigogo vingine viwili ambavyo hadi sasa havina uhakika wa kutinga robo fainali ni MC Alger ya Algeria na Zamalek ya Misri zilizo kundi linaloongozwa na Esperance ya Tunisia ambayo imeshafuzu huku Teungueth ya Senegal ikiwa imeshatupwa nje.

MC Alger inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi nane inahitaji kupata sare tu dhidi ya Esperance ugenini ili iweze kusonga mbele na vinginevyo inaweza kujikuta ikiaga mashindano hayo.

Kwa upande wa Zamalek walio nafasi ya tatu na pointi zao tano, wanahitajika kuibuka na ushindi kwenye mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya Teungueth na kuomba MC Alger ipoteze ugenini mbele ya Esperance ili iweze kufuzu.