Simba yatinga robo fainali kibabe

New Content Item (1)
New Content Item (1)

SIMBA wamepata ushindi wa bao 4-1 dhidi ya AS Vita katika mchezo wao wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo Simba imetinga hatua ya robo fainali ikiwa imefikisha pointi 13 na kuongoza kundi A wakifuatiwa na Al Ahly wenye pointi nane ambao wametoka sare ya bao 2-2 na Al Merreikh.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Katika kundi hilo, AS Vita na Al Merreikh wameaga mashindano hayo, Vita wamekusanya pointi 4 wakati Al Merreikh wana pointi mbili, timu zote nne zimebakiwa na mechi moja mkononi.

Hata hivyo, mechi zilizobaki hata kama Vita na Al Merreikh mmoja wapo akashinda hata kutoka sare hazitaweza kuzifiki Simba na Al Ahly.


Mchezo ulivyokuwa kwa Mkapa

Simba walikuwa wa kwanza kutengeneza nafasi ya kufunga dakika ya 10 kupitia Chriss Mugalu ambaye alimpigia Clatous Chama pasi ya kisigino na kupiga shuti lenye nguvu hafifu ambalo kipa, Omossala Medjo hakupata wakati mgumu kuudaka.

Dakika 15, Aishi Manula aliiweka Simba salama baada ya kupangua shuti kali alilopiga mshambuliaji wa AS Vita, Fiston Kalala akiwa ndani ya boksi.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Dakika 17, Shomary Kapombe alipiga krosi nzuri iliyomkuta, Mugalu akiwa ndani ya boksi na kupiga kichwa ambacho kilitoka nje, sekunde chache ndani ya dakika hiyo, Bernard Morrison nae alikosa bao baada ya kupiga shuti ambalo lilikwenda kugonga nyavu za nje.

Dakika 26, Ducapel Muloko alipiga shuti kali nje ya boksi ambalo kipa, Manula alilipangua na kuwa kona, dakika nne baadaye Simba walipata bao la kwanza lililofungwa na Luis Miquissone dakika ya 30, ambaye alipiga shuti kali ndani ya boksi akipokea pasi ya chinichini kutoka kwa Morrison.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Ilichukua dakika mbili tangu bao hilo kufungwa, hilo AS Vita walisawazisha kupitia Zemanga Soze ambaye alipiga shuti la mbali ambalo lilimshinda kipa, Manula na kwenda kugonga mwamba kabla ya kuingia nyavuni.

Bao hilo ambalo alifungwa Manula lilikwenda kuharibu rekodi yake ya kucheza mechi nne za hatua ya makundi bila kuruhusu bao la aina yoyote.

Dakika 36, Simba walikosa bao lingine la wazi kupitia Mugalu ambaye alikutana uso kwa uso na kipa, Medjo alipangua shuti la chini chini lililopigwa na staa huyo mwenye mabao mawili katika mashindano haya.

Kabla ya dakika moja ya nyongeza kipindi cha kwanza Simba walipata bao la pili kupitia Chama ambaye alipiga shuti la chini chini lililomshinda kipa As Vita, Medjo.

Kipindi cha pili kilianza kwa As Vita kufanya mabadiliko mawili walitoka, Fiston Kalala na Makabi Glody na nafasi zao waliingia, Tulenge Sindani na Wabantu Kabwe.

Mugalu hakuonekana kuwa na mchezo mzuri kwani mpaka dakika 60, kipindi cha pili alikuwa moja ya wachezaji waliokosa nafasi nyingi za kufunga mabao.

Kutokana na hilo kocha wa Simba, Didier Gomes alifanya mabadiliko dakika 62, aliwatoa Mugalu na Morrison nafasi zao walichukua, Meddie Kagere na Rally Bwalya.

Dakika 63, As Vita walifanya mabadiliko alitoka Amede Masasi na nafasi yake kuingia, Papy Tshishimbi mchezaji wa zamani wa Yanga.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na tija kwa Simba, kwani iliwachukua dakika tano tu kupata bao la tatu kupitia Rally Bwalya aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Morrison.

Bwalya alifunga bao hilo dakika 67, akipiga shuti kali la chinichini baada ya kuunganisha pasi iliyotoka kwa Chama.

Dakika 71, Chama alikosa bao la wazi akiwa amebaki na kipa baaada ya kupiga shuti na mguu wa kushoto ambalo lilikwenda kugonga nyavu nje, Simba baada ya kupata bao hilo la tatu walionekana kucheza kwa kupigiana pasi ndefu na fupi huku muda ukiwa unaenda.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Simba walifanya mabadiliko ya tatu dakika 79, alitoka, Jonas Mkude na nafasi yake kuingia, Erasto Nyoni.

Dakika 82, Chama alifunga bao la nne ambalo unaweza kuliita la kideoni kwani alifunga kwa mvuto wa aina yake baada ya kuwaahadaa mabeki wa As Vita ambao walikuwa kama wanagalagala chini.

Simba walifanya mabadiliko mengine mawili walitoka Chama na Luis nafasi zao wakachukua, Francis Kahata na Hassan Dilunga, mabadiliko hayo yaliendelea kuimarisha timu hiyo eneo la kiungo na kucheza kwa utulivu.