Simba yapenya kibishi Afrika, sasa kuwavaa Wazimbabwe

Simba yapenya kibishi Afrika, sasa kuwavaa Wazimbabwe

Muktasari:

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba imefanikiwa kusonga mbele kibishi hadi raundi ya kwanza licha ya kulazimishwa suluhu nyumbani na Plateau United ya Nigeria na sasa watavaana na Wazimbabwe, FC Platinum

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba imefanikiwa kusonga mbele kibishi hadi raundi ya kwanza licha ya kulazimishwa suluhu nyumbani na Plateau United ya Nigeria na sasa watavaana na Wazimbabwe, FC Platinum
Haikuwa kazi nyepesi kwa Simba kutinga raundi hiyo ya kwanza kwa faida ya bao la ugenini iliposhinda 1-0 ikiwa mjini Jos, Nigeria kutokana na wageni wao Plateau United kuupiga mpira mwingi na kuwabana Wekundu wa Msimbazi ambao walitawala zaidi katika kipindi cha pili.
Kwenye mechi hiyo iliyopigwa jioni hii Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Simba ilipambana kiume kuwabana wageni hao waliotawala kipindi cha kwanza hsa kwa kupiga pasi mwanzo mwisho japo walishindwa kutumia nafasi walizopata.

DAKIKA 45 ZA KWANZA
Plateau iliivuruga Simba, ilicheza kwa kulinda kuanzia eneo  la kiungo ambapo ilitumia mfumo wa 4-2-3-1 na kuwafanya Wekundu wa Msimbazi, ikicheza kwa kupooza kutokana na eneo lao la kati kutibuliwa na mfumo huo.
Simba ikiongozwa na viungo Jonas Mkude na Mzamiru Yassin ikifichwa na kiungo wa Plateau United, Isah Ndala aliyekuwa anatibua mipango yote ya Simba  katikati ya uwanja, japo beki wa kushoto Mohamed Hussein 'Tshabalala' na winga Luis Miquissone walionyesha uhai wa kutengeneza mashambulizi kwao.
Dakika 10 kabla ya kumaliza kipindi cha kwanza Plateau ilibadili mfumo na kucheza 4-4-2.
Wakati kwa upande wa Simba kocha Sven naye alikichezesha kikosi chake kwa kubadili mifumo kuna wakati kilikuwa kinacheza 4-2-3-1 na 4-3-3.
Lakini pia dakika za kipindi cha kwanza mechi haikuwa na mvuto kutokana na Plateau United kujiangusha angusha chini mara kwa Mara kila walipokuwa wakiguswa na wachezaji wa Simba.
Ukiachana na hilo changamoto ambayo walikuwa wanaipata Simba wakipata mipira ya kona na faulo ni kutokana wachezaji wengi kuwa na kimo kifupi tofauati na wapinzani wao ambao wengi walikuwa warefu na kutumia Sana mipira ya juu ambayo mchezaji pekee wa Simba aliyeweza kumudu mipira hiyo ya juu alikuwa nahodha John Bocco.

KIPINDI CHA PILI
Simba ilianza kwa kasi iliyowalazimisha Plateau United kufunguka ikitaka kujizuia na kushambulia kwa kushitukiza.
Huku mabadiliko aliyoyafanya Sven ya kumtoa Dilunga na kumuingiza Benard Morrison yalisaidia safu ya mbele kuchangamka na kusababisha faulo mara kadha.
Dakika ya 64 Miquissone aliambaa na mpira kutoka eneo la katikati lakini bahati mbaya shuti lake halikuwa na madhara.
Kwa matokeo hayo Simba sasa itacheza na Platinum iliyoshinda nyumbani mabao 2-0 dhidi ya Costa do Sol ya Msumbiji na kuing'oa kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya mechi ya awali ugenini kuwafumua 2-1. Timu hiyo ya FC Platinum inachezewa na straika wa zamani wa Simba, Elias Maguri na ilishawahi kuja nchini kuvaana na Yanga na kufumuliwa mabao 5-1 kabla ya kushinda kwao bao 1-0 katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika 2015.
Kikosi cha Aishi Manula, Shomari Kapombe,Mohammed Hussein,Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude,Clatous Chama,  Mzamiru Yassin,John Bocco, Hassan Dilunga na Luis Miquissone.

Na OLIPA ASSA NA OLIVER ALBERT