Simba, Yanga zapewa mchongo CAF

Muktasari:

  • Simba na Yanga ndizo zinawakilisha Tanzania katika michuano hiyo zikiweka rekodi msimu huu ya kuwa nchi pekee ambayo imeingiza timu mbili kwenye hatua ya makundi.

WAKATI Simba na Yanga zikiendelea kuchora ramani ya kuwamaliza wapinzani wao kwenye michezo ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, nyota wa zamani wa timu hizo, Willy Martin ‘Garikubwa’ amewapa maujanja ya kumaliza kazi mapema.

Simba na Yanga ndizo zinawakilisha Tanzania katika michuano hiyo zikiweka rekodi msimu huu ya kuwa nchi pekee ambayo imeingiza timu mbili kwenye hatua ya makundi.

Simba ambayo ni msimu wa nne mfululizo kutinga hatua hiyo watawakaribisha Al Ahly, mchezo ukipigwa Ijumaa, huku Yanga wao wakiwavaa Mamelodi Sundowns Jumamosi, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Mkapa.

Garikubwa alisema pamoja na ugumu wa mechi hizo, lakini anayo matumaini kwa wawakilishi hao wa Tanzania kufanya vizuri huku akiwapa siri namna ya kuvuka hatua hiyo.

Alisema Simba na Yanga zina vikosi bora vya kuweza kuamua matokeo, hivyo wanapaswa kupambana kupata mabao ya mapema ili kuwatoa mchezoni wapinzani, lakini kutokubali kuchezea mipira eneo la hatari.

“Uhakika timu hizo zitashinda, lakini lazima wapambane kupata mabao ya haraka, idadi iwe zaidi ya mawili lakini wajiamini wanapokuwa uwanjani kwani wapo nyumbani,” alisema Garikubwa.

Nahodha huyo wa timu hizo aliwataka Henock Inonga na Che Malone (Simba) na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Dickson Job wa Yanga kuwa makini kutokana na timu pinzani kuwa na mpira wa mashambulizi muda mwingi na hivyo wahakikishe hawakai sana na mpira langoni kwao.