NOTI ZITAONGEA: Mastaa Ligi Kuu watakaokuwa ghali sokoni

Muktasari:

  • Vigogo vya soka la Bara, Simba na Yanga kwenye vikosi kuna mastaa wanaomaliza mikataba mwishoni  mwa msimu huu na baadhi yao ni muhimu katika timu hizo.

SINEMA inayoendelea ya mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis kudaiwa kugoma kuongeza mkataba mpya ndani ya kikosi hicho inatoa picha jinsi shughuli inavyoweza kuwa pevu kwa viongozi wa timu mbalimbali kuwabakisha mastaa wao.

Vigogo vya soka la Bara, Simba na Yanga kwenye vikosi kuna mastaa wanaomaliza mikataba mwishoni  mwa msimu huu na baadhi yao ni muhimu katika timu hizo.

Mfano mzuri ni Kibu ambaye anatolewa macho na  Yanga pamoja na Ihefu kiasi cha vigogo wa Simba kuanza haraka mazungumzo naye tofauti na awali ambapo walipanga kufanya mazungumzo baada ya msimu kumalizika.

Inadaiwa kwamba Yanga na Ihefu zimemtangazia ofa nono mshambuliaji huyo ambaye alikuwa kipenzi cha  kocha wa zamani Msimbazi, Mbrazili Robetto Oliveira ‘Robertinho’.

 Wafuatao ni mastaa ambao wanaweza wakawa na bei mbaya sokoni, kulingana thamani ya kile wanachoonyesha uwanjani, huku wengine wakiwa katika rada za timu mbalimbali.


AZIZ  KI (YANGA)

Kama Yanga itakuwa haijamuongezea mkataba Aziz Ki ni kati ya mastaa wanaoweza kuwa ghali sokoni kwani hadi sasa katika mechi zinazoendelea za Ligi Kuu Bara ndiye anaongoza kwa kufunga akiwa na mabao 15.

Ingawa za ndaaani kabisa zinaeleza kwamba tayari Aziz Ki kamalizana na Yanga akiwa amewakamua pesa ndefu, huku taarifa nyingine zikielezwa Azam na Simba nazo zimeweka nia juu yake. Hapo kitakachoamua ni nani mwenye kisu kikali cha kukata nyama.


CLATOUS CHAMA (SIMBA)

Kiungo wa Simba, Clatous Chama anadaiwa kutakiwa na Yanga na tetesi juu yake hazijaanza msimu huu kwani zilikuwepo kabla ya dili lake la kusajiliwa na RS Berkane ya Morocco (2020/21) ambao alimaliza na mabao manane na asisti 15. Msimu huu Chama keshafunga mabao saba na asisti sita. Taarifa za kuhusishwa na Yanga zimekuwa kubwa kuliko anavyotajwa kuhitajika Azam na kusalia kwenye kikosi cha Simba. 


KIBU DENIS (SIMBA)

Sinema  ya mshambuliaji Kibu Denis imenoga. Wakati Simba ikipambana kumbakiza kikosini kuna timu zinazompigia hesabu kali na taarifa zilizopo ni kwamba kawekewa vibunda vya maana mezani. Timu zinazotajwa ni Yanga na Ihefu na mkataba wake unaishia mwisho wa msimu huu.

BAKARI MWAMNYETO (YANGA)

Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto ni kati ya mastaa wanaomaliza mkataba mwishoni mwa msimu huu, lakini bado klabu yake inadaiwa kwamba haijakaa naye mezani, huku zikiwepo tetesi za Simba kuitaka huduma yake.

Katika msimu wa 2020/21 wakati anajiunga na Yanga akitokea Coastal Union huduma yake ilikuwa inawaniwa na Simba pia. Hivyo kuhusishwa na wana Msimbazi siyo kitu kipya.


KIBWANA SHOMARI (YANGA)

Pamoja na changamoto ya namba ambayo amekuwa akikumbana nayo mbele ya Attohoula Yao (26), Kibwana ni kati ya mabeki bora wazawa upande wa kulia na msimu uliopita aliisaidia Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mwamnyeto ni kati ya wachezaji wenye thamani na amekuwa akithibitisha hilo  pale ambapo amekuwa akipewa nafasi mfano mzuri ni katika mchezo uliopiwa wa Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Tabora United. Miongoni mwa timu ambazo zinamfuatilia beki huyo ni pamoja na Azam.

Kibwana ameshazungumzia hilo akisema, “kwa sasa ni mchezaji wa Yanga. Ni kweli kuna timu nyingi zimeleta ofa, ila nawapa nafasi kubwa waajiri wangu.”


FARID MUSSA (YANGA)

Huyu ni kati ya wachezaji ambao wamekuwa wakitajwa kuwa na kipaji kikubwa na uwezo wake wa kucheza nafasi tofauti  kama beki wa kushoto ni miongoni mwa mambo ambayo yanamfanya kuwa na thamani.

Licha ya kutokuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza Yanga, Ken Gold na Azam ni kati ya timu ambazo zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili nyota huyo ambaye aliwahi kucheza soka la kulipwa Hispania katika timu ya CD Tenerife.


SAID NTIBAZONKIZA ‘SAIDO’ (SIMBA)

Licha ya kutajwa umri wa soka kumtupa mkono, Saido ni kati ya wachezaji wenye uzoefu mkubwa na anaonyesha kuwa ana uwezo wa kuendelea kucheza soka la ushindani kama ilivyo kwa nahodha wa zamani wa Yanga, Kelvin Yondan anayecheza Geita Gold. Miongoni mwa timu ambazo amekuwa akihusishwa nazo zipo za nyumbani kwao Burundi na APR ya Rwanda ambayo ina wachezaji wa zamani wa Simba, Sharaf Shibob na Taddeo Lwanga ambao msimu huu wameiwezesha kutwaa ubingwa wa ligi.


HENOCK INONGA (SIMBA)

Ni kama ndoa ya beki Inonga na Simba ipo ukingoni kutokana na kudaiwa kuwa Mkongomani huyo ameshasaini mkataba wa awali na FAR Rabat inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi.

Inasemekana kuwa beki huyo alisaini baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zilizofanyika nchini Ivory Coast mwanzoni mwa mwaka huu.

Hata hivyo, kutokana na mkataba wake kuwa ukingoni na iwapo hajaini kokote huenda akagonganisha vigogo milango ya usajili itakapofunguliwa.

Wachezaji wengine ambao mikataba yao ipo ukingoni na wanaweza kushawishi timu kuwasajili ni Metacha Mnata, Jonas Mkude na Skudu Makudubela (Yanga) pamoja na Sadio Kanoute (Simba).

Akizungumzia timu yake, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally anasema: “Licha ya timu yetu kusemekana ni mbovu lakini ndio inayoongoza kwa wachezaji wake kuhitajika na klabu nyingi zaidi za ndani na nje nchi. Ni dhahiri kuwa tuna kikosi chenye wachezaji bora. “Hatujapata matokeo mazuri msimu huu lakini haiondoi ukweli kuwa wachezaji wetu ni bora sana ndio maana wanatajwa sana sokoni. Tunachoenda kukifanya hivi sasa ni kubaki na wale bora wenye moyo wa kuitumikia Simba.”

Kocha mkongwe, Sunday Kayuni anasema: “Kuondoka wachezaji hao ndani ya klabu hiyo siyo shida ila ni namna viongozi watakavyopata mbadala wao. Pia itategemeana na mifumo ya makocha wao.” Beki wa zamani wa Simba na Stars, Boniface Pawasa anasema: “Kutokana na uwezo walioonyesha watakuwa ghali.