Simba, Yanga wanavyoishi kishua Dar

Muktasari:

  • Mara kadhaa unaweza kuwakuta kwenye vijiwe vikubwa vya jiji la Dar es Salaam wakila maisha mazuri na kutanua ndiga kali kutokana na fedha ambazo wamekuwa wakilipwa hata wakati mwingine mafanikio yao ambao yanawakosha wadau wao

MASTAA wa soka ni kati ya watu ambao wamekuwa wakiishi maisha ya kifahari kutokana na kiwango cha fedha ambacho wamekuwa wakilipwa.

Wachezaji wengi wamekuwa wakipata fedha nyingi kwa sasa kutokana na uwekezaji ambao umekuwa ukifanywa hususani kwa Simba na Yanga ambazo msimu huu zimepiga hatua hata kimataifa.

Mara kadhaa unaweza kuwakuta kwenye vijiwe vikubwa vya jiji la Dar es Salaam wakila maisha mazuri na kutanua ndiga kali kutokana na fedha ambazo wamekuwa wakilipwa hata wakati mwingine mafanikio yao ambao yanawakosha wadau wao.

Lakini pia mastaa hao wanakula maisha mazuri kutokana na mikataba mikubwa ambayo wamekuwa wakisaini na timu zao, wengi wakihusisha magari makali pamoja na mazingira mazuri ya kuishi.

Wapo pia ambao mikataba yao inahusisha elimu kwa watoto wao, lakini tiketi za ndege kuja na kurudi kwao mara mbili au tatu kwa mwaka na maisha yanasonga.

MAISHA YAO YALIVYO

Leo tutaangalia maisha safi wanayoishi mastaa mbalimbali wa Simba na Yanga hapa jijini Dar es Salaam. Wachezaji hawa wamekuwa wakiishi kwenye majumba ya kifahari na kuwashinda hata wafanyakazi wa makampuni makubwa hapa nchini (Hatutataja majina ya majengo hayo kutokana na sababu za kiusalama za wachezaji hao).

Tofauti ya Simba na Yanga ni kwamba, Simba wao wanawatafutia mastaa wao nyumba na wanakaa sehemu moja wengi lakini penye kiwango.

Yanga wao humpa kila mchezaji mgeni dola 500 (Sh1.7Milioni) kwa mwezi kwa ajili ya nyumba. Kama mchezaji  ataona ni kitita kidogo au haiendani na nyumba anayotaka huiingia mfukoni kwake na kuongeza.

MAYELE

Huyu ni mshambuliaji wa Yanga ambaye amekuwa akifanya vizuri msimu huu akitokea DR Congo, ndiye mfungaji bora kwenye Ligi Kuu msimu huu hadi sasa akiwa amepachika mabao 16.

Ukiachana na Ligi, Mayele anaongoza pia kwenye kupachika mabao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na mabao sita na pasi tatu za mabao.

Huyu anaishi kwenye Apartment maeneo ya Victoria, Kijitonyama Jijini Dar es Salaam. Mwanaspoti linajua kuwa sehemu ambayo mchezaji huyo anakaa na familia yake na analipa dola 800 ambayo ni sawa na shilingi milioni 2. Ana gari kali aina ya Toyota Harrier nyeusi  na Toyota Premio.

KHALID AUCHO

HUYU ni kiungo wa Yanga raia wa Uganda ambaye amefanya kazi kubwa kwenye mafanikio ya timu hiyo msimu huu.

Aucho ni kati ya wachezaji wanaotumia magari ya kifahari akiwa jijini Dar es Salaam ambapo anaendesha BMW X5, lakini anaishi  Mikocheni jirani na Hospitali ya TMJ, ambayo chanzo chetu kimetuonyesha kuwa jamaa analipiwa dola 700 kwa kila mwezi. Sawa na Sh1.7Milioni.

AZIZI KI

Ni kiungo mshambuliaji raia wa Ivory Coast akiwa anatajwa kati ya wachezaji ambao walisajiliwa kwa kitita kikubwa cha fedha.

Huyu anaishi kwenye mjengo Kawe Mzimuni, lakini tofauti kwake ni kwamba anakaa sehemu kubwa zaidi na analipa dola 800 sawa na Sh2 kwa mwezi. Anatumia magari ya Benard Morrison mara kwa mara au magari ya kukodisha. Ni mchezaji ambaye anaishi kimahesabu sana, hapendi makuu.

Anaishi kwenye eneo moja na  kipa mahiri zaidi hapa nchini Djigui Diarra ambaye amefanya vizuri kwenye ligi na michuano ya kimataifa mwaka huu.

Huyu ni raia wa Mali naye anaishi kwenye eneo ambalo analipa dola 800 (Sh2milioni) kwa mwezi, lakini akiwa hana gari kama alivyo KI, naye mara nyingi mtaani amekuwa akitumia magari ya Morrison ambaye wanaishi naye sehemu moja akiwa analipa kiwango hicho cha fedha.

 YANICK BANGALA

Bangala mbali na kucheza kwenye eneo la kiungo amekuwa pia na mhimili mkubwa sana kwenye eneo la ulinzi la timu hiyo ya Jangwani akiwa anaishi pia kwenye mejngo mmoja wa maana Mikocheni, Jijini Dar es Salaam ambayo inamlazimsha kukunjua dola 700 kila mwisho wa mwezi kulipa eneo hilo. Ni kama Sh1.7 kwa mwezi.


ClATOUS CHAMA

Amekuwa akitajwa kati ya wachezaji bora sana kwenye timu hiyo akiwa amepangiwa na Simba ghorofa moja matata eneo la Mikocheni Jijini Dar es Salaam  ambapo uchunguzi umeonyesha kuwa analipa dola 800 kwa mwezi sawa na Sh2milioni.

Chama raia wa Zambia anakaa na watoto wake watatu pamoja na mchumba wake. Staa huyo mwenye upande wa gari anatajwa kuwa mmoja kati ya watu wanaotumia magari ya beki ghali zaidi, kwa sasa akiwa anatumia Range Rover na BMW kwenye mihangaiko yake ya jiji la Dar es Salaam, lakini chanzo kinasema kuwa magari hayo ndiyo pia amekuwa akitumia akiwa kwao Zambia.

MOSES PHIRI

Huyu ni Mzambia mwingine ambaye anaishi nyumba moja na Chama, Phiri mwenye mabao 10 kwenye Ligi Kuu Bara naye anaishi Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji huyo anaishi na familia yake, akiwa na mke na watoto wawili na chanzo kinaonyesha kuwa kwenye ghorofa hilo lililopo Mikocheni analipa kiwango kilekile kama cha Chama cha dola 800 kwa mwezi, lakini ikionekana kuwa hana gari analomiliki jijini Dar es Salaam zaidi ya kuonekana mara kwa mara akiwa na magari ya Chama au usafiri wa kukodi.

JONAS MKUDE

Huyu anaishi maeneo ya Kimara jijini Dar es Salaam akiwa ni mmoja kati ya wachezaji ambao wamejenga majumba ya kisasa hapa Dar.

Mkude pamoja na kwamba hajapata nafasi ya kucheza mara kwa mara msimu huu, lakini anaishi kwenye nyumba ya kishua, pamoja na kwamba kwenye kipengele cha mkataba wake na Simba kuna sehemu anatakiwa kulipiwa kodi.

Kwa upande wa ndinga Mkude raia wa Tanzania amekuwa akitanua mtaani na gari kali aina ya Toyota Harrier.

SADIO KANOUTE, BANDA,SAKHO, BALEKE

Simba imekuwa na utaratibu mara kwa mara wa kuwatafutia baadhi ya mastaa wao sehemu za kuishi na wachezaji wengi wa timu hiyo wanaishi kwenye Apatimenti maeneo ya Mbezi jijini Dar es Salaam. Hizi ni za kishua Zaidi.


Kundi kubwa la wachezaji wa Simba pamoja na baadhi ya watu wa benchi la ufundi wanaishi kwenye eneo hilo ambalo inaidaiwa kuna makubaliano maalumu kati ya timu hiyo na uongozi wa Apatimenti hiyo.

Chanzo kinaonyesha kuwa kila mmoja analipa kitita cha dola 700 kwa mwezi mmoja. Sawa na Sh1.6Milioni.

Mastaa wanaoishi hapo ni Sadio Kanoute, Peter Banda, Pape Sakho, Jean Baleke Augustine Okrah na wengine wengi wanaotoka nje ya nchi.

Mastaa hawa wa Simba kwenye usafiri wengi wamekuwa wakikodi kutoka kwenye makampuni mbalimbali, lakini wakati mwingine wamekuwa wakitumia ya wachezaji wenzao au marafiki. Ingawa Mwanaspoti linajua kwamba kwenye mikataba yao kuna sehemu kuna makubaliano ya kupewa gari ila baadhi yao hutaka kupewa fedha tasilimu na kuweka mifukoni na kutumia wa kukodi.