Simba, Yanga wafunguka kuahirishwa Kariakoo Derby

KUAHIRISHWA kwa pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga lililopangwa awali kupigwa Oktoba 18 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kumezua gumzo, wadau wakiishangaa Bodi ya Ligi (TPLB) kwa panga pangua isiyoisha huku makocha wa timu mbalimbali wakilalamikia hali hiyo.

Hata hivyo, Bodi ya Ligi imesisitiza wameahirisha mechi hiyo kwa sababu ya michezo ya kimataifa ya timu za taifa na kwamba tarehe mpya iliyopangwa ya Novemba 7 mechi itapigwa kama ilivyopangwa licha ya Stars kuwa na pambano la mechi za makundi ya kuwania ushiriki wa fainali za Afcon 2021 dhidi ya Tunisia.

Mechi ya Stars na Tunisia ambazo zipo Kundi J sambamba na Libya na Guinea ya Ikweta, zitavaana kwenye mechi yao ya raundi ya tatu Novemba 13 mjini Tunis, Tunisia kabla ya kurudiana Novemba 17 jijini Dar es Salaam, jambo linaloleta hofu huenda ratiba ya kambi ya Stars kuingilia tena pambano hilo la watani.

Wakati mashabiki wa timu zote mbili wakitambiana kila mmoja akimkebehi mwenzake anajichelewesha kwa kipigo baada ya mechi kusogezwa, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema wameupokea kwa mikono miwili uamuzi wa kusogezwa mbele mechi hiyo.

“Tunaheshimu mamlaka katika hilo, ingawa tulijipanga kushinda Oktoba 18, ila tutaendelea kujipanga kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi,” alisema.

Kwa upande wa Yanga wao, kupitia Ofisa Habari wao, Hassan Bumbuli alisema uongozi wao umepokea kwa mikono miwili uamuzi huo na wanaheshimu mamlaka na wanakiandaa kikosi chao kwa tarehe nyingine ya pambano hilo sambamba na mechi nyingine za ligi hiyo.

“Huu ndio msimamo wetu, tumeridhia na kuheshimu uamuzi huo na tunajipanga kwa mechi nyingine kabla ya kuvaana na watani wetu, moto wetu ni ule ule kama wa msimu uliopita,” alisema Bumbuli.

VIGOGO WASHANGAA

Kuahirishwa kwa mechi hiyo kumewashangaza vigogo wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakihoji waliofanya uamuzi huo wamepitia kalenda ya Shirikisho la soka la kimataifa (Fifa) na lile la Afrika (CAF).

Angetile Osiah, Katibu Mkuu wa zamani wa TFF alisema kalenda ya Fifa na CAF ndizo zinazotoa muongozo wa mpangilio mzuri wa ratiba za ligi ya ndani ili kuepusha muingiliano wa ratiba.

“Sina uhakika kama waliofanya uamuzi huo walikuwa na kalenda za mashirikisho hayo ya kimataifa,” alisema Angetile, huku Mkurugenzi wa Ufundi wa zamani wa TFF, Sunday Kayuni, alisema katika hilo, kuna mahali inaonyesha hakuna weledi.

“Kalenda ya Fifa inajulikana na sheria zake ziko wazi, inabidi kuzifuata ili kutoharibu ratiba ya ligi, japo TFF iko sahihi kwa hiki ilichokifanya,” alisema Kayuni.

Naye Mkurugenzi wa zamani wa Mashindano wa TFF na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba alisema mechi ya timu ya taifa inapaswa kupewa thamani yake ipasavyo.

“Awali ratiba ya mechi ya Stars na Tunisia ya kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ilikuwa ichezwe Novemba 9 na kupata wasiwasi, ila nasikia wamesogeza hadi Novemba 13, hivyo nadhani mechi ya watani Novemba 7 itabaki kama ilivyopangwa,” alisema Kawemba.

MAKOCHA WAJA JUU

Kuahirishwa kwa mechi hiyo na baadhi ya mechi za Ligi kumetajwa kuwa changamoto pia kwa klabu nyingine, ikielezwa hazigusi Simba na Yanga tu bali hadi timu nyingine za ligi hiyo.

Kocha Khalid Adam wa Mwadui anasema mabadiliko hayo yamekuwa yakiziumiza klabu, ikiwamo wao ambao mechi yao ya Oktoba 9 na Azam imesogezwa hadi Oktoba 15.

“Tuko njia panda, hatujui kama tuendelee kubaki Dar es Salaam hadi Oktoba 15 au turudi Shinyanga,” alisema.

Mapema jana asubuhi, TPLB ilitoa taarifa za kuahirishwa kwa mchezo huo wa duru la kwanza kwa watani na wa 105 baina yao kwenye Ligi ya Bara tangu 1965, kwa kuhofia kuwepo changamoto ya usafiri kwa baadhi ya wachezaji waliokwenda kuzitumikia timu zao za taifa.

Nyota watatu wa Simba walioitwa katika timu zao, ni Luis Miquissone (Msumbiji), Joash Onyango (Kenya) na Meddie Kagere (Rwanda), huku Francis Kahata, Clatous Chama na Larry Bwalya wakiondolewa kwa sababu mbalimbali na kwa upande wa Yanga hakuna nyota wa kigeni walioitwa.

Licha ya Bodi kueleza mechi imeahirishwa kwa sababu walizotoa, mmoja wa viongozi waandamizi wa michezo nchini (jina limehifadhiwa) alisema kwa kifupi juu ya kuahirishwa kwa mechi hiyo;

“Japo Bodi na TFF imeeleza sababu ya kusogezwa mbele mechi hiyo, lakini kikubwa kilichochangia nafikiri ni masuala ya uchaguzi mkuu, unajua Simba na Yanga sawa ni klabu za mpira, lakini zina siasa.”

Mwandamizi huyo alisema kwa sasa nchi iko kwenye jambo kubwa la uchaguzi mkuu, hivyo matokeo ya mechi kwa namna moja au nyingine yangeweza kuingilia masuala ya uchaguzi mkuu.