Simba, Yanga vita nzito

Muktasari:

ACHANA na vita ya ufungaji, katika Ligi Kuu Bara kwa sasa kuna vita nzito baina ya vigogo Simba na Yanga zikichagizwa pia na Azam FC katika mbio za ubingwa wa msimu wa 57 tangu ligi hiyo ilipoasisiwa mwaka 1965.

ACHANA na vita ya ufungaji, katika Ligi Kuu Bara kwa sasa kuna vita nzito baina ya vigogo Simba na Yanga zikichagizwa pia na Azam FC katika mbio za ubingwa wa msimu wa 57 tangu ligi hiyo ilipoasisiwa mwaka 1965.

Baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mwadui mjini Shinyanga, watetezi Simba ina mechi 12 mkononi, ikiwa imeshacheza michezo 22 kati ya 34 ya msimu huu na kukusanya pointi 52, huku vinara Yanga wakiongoza msimamo na alama zao 54 baada ya mechi 25, ikisaliwa na mechi 9 tu.

Azam iko nafasi ya tatu imekusanya pointi 50 kupitia michezo 26, ikiwa na maana mikononi imesaliwa na mechi nane tu kufunga hesabu za msimu huu.

Kwa hesabu za haraka zilivyo ni kwamba kama Simba itashinda mechi zake zote ina uwezo wa kukusanya pointi ambazo hazitawezwa kufikiwa na timu yoyote na kutetea taji kwa msimu wa nne mfululizo, ila kama itateleza na Yanga au Azam wakafanya kweli zinaweza kubeba.

Lakini wakati Simba imetazamwa kuwa na uwezo wa kushinda kila mechi kutokana na aina ya kikosi chake kuwa na ushindani kila idara, Yanga imeshauriwa kujikita katika kujenga kikosi bora kitakachotesa kwa misimu ijayo endapo watawaacha wachezaji wakae kwa pamoja kwa muda mrefu.

Mwanaspoti limekuchambulia michezo iliyobaki kwa timu hizo na alama zitakazokusanya, huku wadau wakitoa mitazamo yao kulingana na mienendo ya klabu hizo, huku Simba ilipewa nafasi kubwa ya ubingwa endapo tu itashinda yote.

Simba ikishinda mechi zote 12 ilizobakiwa nazo mkononi itakusanya pointi 36, hivyo zikichanganywa na ilizokuwa nazo kwa sasa yaani 52, ina maana itamaliza msimu na jumla ya pointi 88 zikiwa ni nyingi kufikiwa na wenzake.

Hata hivyo, hii inategemea na kama itashinda zote ukiwamo ule wa watani wao, Yanga unaotarajiwa kupigwa Mei 8, kwani tayari ameshamalizana na Azam na kushinda moja 4-0 na mwingine kutoka sare ya 2-2.

Simba imeshinda mechi 16 katika michezo 22 iliyocheza, ikipata sare nne nakupoteza mara mbili, ikiwa na maana imedondosha pointi 14 tu, ikiwa na michezo mitatu mkononi kuifikia Yanga iliyocheza 25 na kukusanya alama 54.

Yanga yenyewe imesaliwa na michezo tisa baada ya juzi kushinda 1-0 dhidi ya Biashara United na kama itakomaa na kushinda zote ikiwamo dhidi ya Simba na Azam watakaovaana wakirudi kutoka kwenye mechi ya Kombe la ASFC, itapata pointi 27 ambazo zikijumuishwa na ilizonazo sasa yaani 54 itamaliza msimu na alama 81.

Katika mechi zake 25 za awali, Yanga imeshinda 15 kutoka sare 9 na kupoteza mchezo mmoja, ikipoteza jumla ya pointi 21 katika mechi zake za sasa, ilihali Azam FC ambayo ina pointi 50 katika mechi zao 26, ikishinda 14, sare nane na kupoteza nne. Ikishinda zote zilizobaki itamaliza msimu kwa alama 74 tu.