Simba, Yanga usiku freshi

KUMBUKUMBU ya mechi tano zilizopita za mashindano ya kimataifa ambazo Yanga na Simba zilicheza usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa zinazipa jeuri ya kufanya vyema katika mechi za kwanza za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly na Mamelodi Sundowns, Ijumaa na Jumamosi wiki hii uwanjani hapo.

Timu hizo mbili za Tanzania, zimeonekana kuwa na historia nzuri ya mechi za usiku za mashindano ya kimataifa kwa siku za hivi karibuni huku wageni wakikiona cha mtema kuni.

Katika mechi tano zilizopita za mashindano ya kimataifa ambazo Simba imecheza usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, imeibuka na ushindi mara tatu, kutoka sare moja na kupoteza mchezo mmoja.

Mechi za usiku ambazo Simba ilipata ushindi kati ya hizo tano zilizopita ambazo ilicheza usiku, ni dhidi ya Jwaneng Galaxy ambayo ilikuwa ya mwisho ya hatua ya makundi msimu huu ambapo ilipata ushindi mnono wa mabao 6-0, yaliyopachikwa na Clatous Chama, Omar Jobe, Ladack Chasambi, Kibu Denis, Saido Ntibazonkiza na Fabrice Ngoma.

Kabla ya hapo, Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 katika mechi ya robo fainali ya mashindano ya African Football League (AFL) dhidi ya Al Ahly, kwa mabao ya Sadio Kanoute na Kibu Denis.

Mechi nyingine mbili ambazo ilipata ushindi usiku zilikuwa ni hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita dhidi ya Horoya ambao iliibuka na mabao 7-0 na dhidi ya Vipers iliyoshinda bao 1-0 lakini ilichapwa mabao 3-0 na Raja Casablanca.

Mechi dhidi ya Horoya, mabao saba ya Simba yalifungwa na Clatous Chama aliyepachika matatu na Sadio Kanoute na Jean Baleke ambao kila mmoja alifunga mawili huku bao moja la mechi dhidi ya Vipers likifungwa na Chama.

Kwa upande wa Yanga, katika mechi tano zilizopita ambazo ilicheza usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ilipata ushindi mara tatu na kutoka sare mbili.

Mchezo ambao iliibuka na ushindi mkubwa ni ule ambao iliichapa CR Belouizdad kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambapo ilishinda mabao 4-0 yakipachikwa na Mudathir Yahya, Kennedy Musonda, Stephane Aziz Ki na Joseph Guede na kabla ya hapo ilitoka sare ya bao 1-1 na Al Ahly, bao lake lilipachikwa na Pacome Zouzoua.

Katika mechi nyingine ya usiku, ilitoka sare ya bila kufungana na Rivers United katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na iliichapa Monastir kwa mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa usiku ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, ikipata mabao yake kupitia kwa Kennedy Musonda na Fiston Mayele.

Yanga pia iliichapa Real Bamako kwa mabao 2-0 katika mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita mabao yakifungwa na Fiston Mayele na Jesus Moloko.

Wakati Simba na Yanga zikionekana kutamba nyumbani zinapocheza mechi za usiku katika mashindano ya kimataifa, mambo yanaonekana kutokuwa mazuri kwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ambayo yenyewe imekuwa haina bahati na mechi za usiku.

Katika mechi tano za kimashindano ambazo Taifa Stars ilicheza usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, imepata ushindi mara moja tu, ikitoka sare moja na kupoteza michezo mitatu.