Simba, Yanga ubabe ubabe

Unguja. Si Yanga wala Simba aliyeweza kutikisa nyavu za mpinzani wake katika dakika 45 za kipindi cha kwanza kwenye fainali za Kombe la Mapinduzi zinazofanyika Uwanja wa Amaan kisiwani hapa.

Timu hizo ambazo ni watani wa jadi kutoka mitaa ya Kariakoo jijini Dar es Salaam huku timu hizo zikicheza kwa kushambuliana na mpira kuonekana kuwa na presha kubwa.

Dakika ya sita tu tangu kuanza kwa mchezo huo Miraji Athuman wa Simba alikosa bao akiwa amepiga shuti kali lililogonga mwamba na kutoka nje huku dakika tatu baadaye Saidi Ntibanzonkiza akipiga mpira uliompata Michael Sarpong aliyepaisha juu ya goli.

Safu ya Yanga ilionekana kutokuwa makini katika umaliziaji kwani Sarpong aliinyima tena timu yake bao dakika ya 25 baada ya kupiga mpira uliookolewa na kipa wa Simba, Beno Kakolanya baada ya mabeki wake kupoteza umakini wa kulinda hatari hiyo.

Mwamuzi wa mchezo huo, Nassir Salum Siahi alitoa kadi za njano kwa wachezaji watatu wa timu hizo akianza na David Kameta 'Duchu' baada ya kucheza rafu dakika ya 28 wakati Haruna Niyonzima wa Yanga naye akipewa kadi dakika ya 32 kwa kumchezea rafu Yassin Mzamiru huku kadi ya mwisho ya kipindi cha kwanza ikienda kwa Kennedy Juma wa Simba aliyemchezea rafu Tuisila Kisinda dakika ya 45.

Simba walikosa bao dakika ya 38 baada ya Francis Kahata kupiga mpira wa kona uliompata Joash Onyango aliyepiga kichwa na kutoka nje kidogo ya goli huku Sarpong akipoteza tena bahati dakika ya 38 baada ya kupiga shuti nje akipokea pasi nzuri ya Kisinda.

Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa hazijafungana huku kila kitu ikionyesha kuwa na kiu ya kutwaa ubingwa huo ambapo mara ya kwanza zilikutana kwenye fainali za mashindano hayo mwaka 2011 ambapo simba waliibuka na ushindi.