Simba, Yanga Mwanza kimyaaa

Muktasari:
Yanga ndio wenyeji wa michezo huo ambao utapigwa saa 11:00 jioni huku Simba ikijivunia rekodi ya ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo wa mwisho kukutana kwa timu hizo.
Wakati wadau wa soka nchini wakisubiri kwa hamu mechi ya watani wa jadi, huko jijini Mwanza bado mashabiki wa Yanga na Simba hawajaonyesha msisimko.
Mchezo baina ya watani hao unatarajia kupigwa leo jioni katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam ukiwa wa kwanza kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu msimu huu.
Mwanaspoti Online imezunguka mitaa ya jiji hilo ikiwamo ofisi za mashabiki wa timu hizo na kukuta pamepoa huku wadau wengine wakiendelea na shughuli zao za kila siku.
Jambo kubwa limeonekana kwa waendesha pikipiki 'Bodaboda' ambao walikuwa wakipishana wakiwa na bendera za timu tofauti katika shughuli zao.
Pia wananchi wengine walionekana kupitapita wakiwa wamevalia jezi za Simba na Yanga lakini wakiwa bize na kazi zao za kujipatia riziki.