Simba, Yanga... Karata ya maamuzi

Usiku wa leo timu za Simba na Yanga kutoka Tanzania zitakuwa na kibarua kizito katika mechi mbili tofauti ambazo zitaamua hatima ya kuendelea kusalia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu au kuaga mashindano hayo makubwa.

Simba na Yanga msimu huu zimetisha kwa kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa pamoja ambapo katika hatua hiyo ya mtoano, Simba ilipangiwa Al Ahly ya Misri huku Yanga ikipewa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Watani hao wa jadi wote walianzia mechi za mkondo wa kwanza nyumbani ambapo hawakupata matokeo bora zaidi kwani Simba ilichapwa bao 1-0 huku Yanga ikibanwa mbavu na mechi kumalizika kwa Suluhu, lakini zikionyesha ubabe kwa kucheza soka safi na kujaza Uwanja wa Mkapa kwa siku mbili mfululizo.

Matokeo hayo ya wikiendi iliyopita yanazifanya timu hizo kuwa na michezo migumu leo ambapo mechi ya kwanza itapigwa Uwanja wa Loftus Versfield wakati Yanga itakapokuwa ikipambana na Mamelodi kuanzia saa 3:00 za usiku, huku Al Ahly na Simba mtanange wao ukipangwa kupigwa kuanzia saa 5:00 usiku kwenye Uwanja wa kimataifa wa Cairo, sehemu ambayo Simba wameshacheza msimu huu.

Yanga ina faida kubwa, kwani suluhu ya 0-0 iliyoipata kwenye mechi ya kwanza kwa Mkapa inaipa jeuri ya kufanya vizuri kwani ushindi au sare ya mabao itaifanya kutinga nusu fainali kwa mara ya kwanza licha ya kwamba Mamelodi nayo imepania kufanya vyema katika mtanange huo itakapokuwa nyumbani.

Kwa Simba yenyewe inahitaji mambo mawili, ushindi wa zaidi ya mabao 2-0, ili iweze kuvuka hatua ya nusu fainali baada ya mechi ya mkondo wa kwanza kupoteza nyumbani kwa bao 1-0.

Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema anaamini kwa kikosi chake wapo tayari kupambana ili kuhakikisha timu inapata matokeo inayoyahitaji.

"Tuko vizuri, kitu kikubwa tunachofanya kwa sasa ni kuwajenga wachezaji kujiamini zaidi kwani hakuna linaloshindikana. Ukiamini kila kitu kinawezekana hivyo na sasa tunaamini tunakwenda kupata ushindi na kusonga mbele," alisema Gamondi. anayetarajia kuwa na nyota wake wote aliowakosa kwenye mechi ya awali kutokana na majeraha wakiwemo Pacome Zouzoua na Khalid Aucho.

Chanzo cha ndani kutoka kwenye mazoezi ya Yanga kinasema kuwa kikosi cha timu hiyo kinaweza kuwa na Aucho pamoja na Pacome ambao wameonekana wakifanya mazoezi kwa nguvu kwa siku zote wakiwa Sauzi.

"Kocha anaweza kuanzishia timu yake kwa Pacome, amekuwa akimpa maelekezo kila mara mazoezini na wakati mwingine amebaki naye mwenyewe wakati wachezaji wengine wakiwa wameondoka, Aucho naye amefanya mazoezi siku zote huku," kilisema chanzo hicho.

Namba zinaonyesha kuwa Yanga ni tishio zaidi ya Mamelodi kwenye eneo la ufungaji, ikiwa kwenye hatua ya makundi ilifunga mabao tisa, huku Mamelodi ikifunga sita, lakini vijana hao wa Gamondi wakiwa na shida kwenye eneo la ulinzi ambapo iliruhusu mabao sita na Mamelodi ikiwa imara baada ya kufungwa mawili tu, hivyo kila mmoja ana sehemu ya kuifanyia kazi.

Zinakutana timu zenye rekodi nzuri, ambapo katika michezo mitano iliyopita Yanga imeshinda minne na kutoka sare mmoja, huku Mamelodi ikishinda mitatu na kutoka sare miwili.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha alisema ni mechi ngumu kwa upande wao lakini wapo tayari kupambana hadi mwisho kuhakikisha wanapata ushindi na kusonga mbele baada ya kukwama kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu.

"Ni mechi ngumu ila tumekuja kupambana. Kikosi kipo tayari kujitoa na kuhakikisha tunapata kile tunachokihitaji hakuna jambo lingine zaidi ya kutafuta mabao tukiwa ugenini baada ya kupoteza nyumbani, kila kitu kinawezekana," alisema kocha huyo ambaye ana kumbukumbu nzuri ya kuifunga Al Ahly bao 1-0, msimu uliopita akiwa na kikosi cha USM Alger na kutwaa taji la CAF Super Cup.

Pamoja na kuwa mechi ngumu kwa pande zote mbili lakini bado historia zinaonesha Simba na Yanga zinaweza kushinda ugenini.

Simba ambayo iliondoka juzi ina uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa, hasa baada ya kukutana na Ahly kwenye michezo saba ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa wametoka sare miwili na kupoteza michezo mitatu na kushinda miwili, kwa mara ya kwanza Ahly iliichapa Simba kwenye Uwanja wa Mkapa wiki moja iliyopita.

Rekodi zinaonyesha kuwa kwenye michezo hiyo, Ahly imeifunga Simba mabao 10, huku vijana hao wa Msimbazi wakifunga mabao matano tu.

Ugenini inawezekana:

Msimu uliopita Yanga ilikuwa ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika na kushinda mechi ngumu ugenini mbele ya Club Africain (1-0), TP Mazembe (1-0), ikashinda 2-0 mbele ya Rivers United ya Nigeria ugenini, kisha 2-1 mbele ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini kisha kuichapa USM Alger bao 1-0 kwenye mechi ya fainali iliyopigwa Algeria licha ya kwamba Waarabu hao walitwaa taji hilo kwa faida ya bao la ugenini baada ya kushinda kwa Mkapa 2-1.

Hata hivyo, kwa upande wa Simba pia msimu uliopita ilionyesha inaweza kushinda ugenini baada ya kuichapa Vipers ya Uganda bao 1-0 katika mechi ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika lakini pia mara ya mwisho ilivyocheza na Al Ahly ugenini Oktoba mwaka jana kwenye michuano ya African Football League mechi ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 na Simba kutolewa kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya 2-2 kwa Mkapa.

Ahly kwenye michezo ya minne iliyopita imeshinda mitatu imepoteza mmoja na kutoka sare mmoja, huku Simba katika michezo minne ikishinda mitatu na kupoteza mchezo mmoja.


Dondoo Mamelodi vs Yanga 2023/2024

Wastani wa kumiliki mpira:

Mamelodi 65.8 vs Yanga 48.6

Wastani wa mashuti kwenye lango

Yanga 5.0 vs Mamelodi 4.7

Wastani wa krosi

Yanga 2.9 vs Mamelodi 2.6

wastani wa kufunga bao

Yanga 1.3 vs Mamelodi 1.0

Pasi za uhakika kwa mechi

Mamelodi 493.6 vs Yanga 348.1



Dondoo Al Ahly vs Simba 2023/2024

Wastani wa kumiliki mpira

Al Ahly 54.9 vs Simba 52.1

Wastani wa mashuti kwenye lango

Simba 4.7 vs Ahly 4.3

Wastani wa krosi

Simba 4.4 vs Ahly 4.0

Wastani wa kufunga bao

Simba 1.3 vs Ahly 1.0

Pasi za uhakika kwenye mechi

Ahly 398.1 vs Simba 318.0