Simba, Yanga dabi nyingine Chamazi

Muktasari:

  • Msimu huu timu hizo zimekutana mara mbili, moja kwenye ligi Mnyama akiondoka na ushindi wa mabao 3-1 yakifungwa na Aisha Mnunka aliyeweka kambani mawili na Vivian Corazone na ile ya Ngao ya Jamii Desemba 9, 2023 ambayo Simba iliitoa Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-4 pale dakika 90 zilipomalizika kwa suluhu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

LIGI Kuu ya Wanawake itaendelea tena kesho kwa michezo miwili kupigwa kwenye viwanja tofauti ikiwemo dabi ya Kariakoo kati ya Simba Queens na Yanga Princess kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 10:00 jioni.

Msimu huu timu hizo zimekutana mara mbili, moja kwenye ligi Mnyama akiondoka na ushindi wa mabao 3-1 yakifungwa na Aisha Mnunka aliyeweka kambani mawili na Vivian Corazone na ile ya Ngao ya Jamii Desemba 9, 2023 ambayo Simba iliitoa Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-4 pale dakika 90 zilipomalizika kwa suluhu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Timu hizo zinakutana tena baada ya miezi mitatu kupita lakini Simba ikionekana kuwa bora zaidi ya Yanga kwani kwenye mechi 11 imeshinda zote na Wananchi wakipoteza mechi tatu dhidi ya Ceasiaa 1-0, Simba na JKT kwa mabao 3-1.

Yanga Princess haijawahi kuifunga Simba Queens ndani ya misimu mitano na mara ya mwisho kushinda ilikuwa ni 2018 wakishinda bao 1-0 lililofungwa na Clara Luvanga aliyetimka Al Nassr ya Saudi Arabia, na msimu huu imefunga mabao 17 na kuruhusu tisa, Simba ikifunga 36 na kuruhusu mabao sita.

Hii ni nafasi kwa mastraika wa timu zote mbili hasa Aisha Mnunka ambaye msimu huu amekuwa bora na kuwania kiatu cha ufungaji bora akiweka kambani mabao 13 mbele ya Stumai Abdallah (JKT Queens) mwenye nayo 16 kwenye mechi 11, lakini kwa Yanga licha ya mastraika wao kutofunga mabao mengi wana viungo Precius Christopher na Saiki Atinuke ambao wana uwezo wa kuamua mechi hiyo.

Huo ni mchezo muhimu kwa Simba ambayo ikishinda itajiweka pazuri kwenye mbio za ubingwa msimu huu kwani ndio inaongoza kwenye msimamo na pointi 31 ikiizidi JKT pointi sita.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, kocha msaidizi wa Yanga Princess, Fredy Mbuna alisema: "Tunajua ni dabi na mechi kubwa na sisi tutaingia kikubwa kwa ajili ya kushinda mchezo huo."

Nahodha wa Yanga Princess, Noela Luhala alisema: "Siku zote mchezo wa dabi ni dabi na presha inakuwapo na tunajua tutapambana ili kuibeba presha hiyo na wachezaji wote wanajua umuhimu wa mechi hiyo."

Kocha Msaidizi wa Simba, Mussa Hassan 'Mgosi' alisema: "Hii ni mechi ambayo kila timu inahitaji ili kufikia malengo yake, kwetu maandalizi yote yapo sawa kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki kwa kumaliza mchezo tukiwa tumeshinda kwani malengo yetu ni kutwaa ubingwa msimu huu."

Nahodha wa Simba, Violeth Nickolaus alisema: "Sisi tunafanya maandalizi siku zote yaani ligi nzima, hatuna majeruhi katika mchezo wa kesho na makosa yaliyojitokeza katika mchezo uliopita yamefanyiwa kazi mazoezini."