Simba, Yanga buana! Kinatoka kitu kinaingia kitu

Muktasari:

  • Yanga imejikuta ikiishiwa pozi kwani wamesaliwa na alama zao 74 katika mechi 32, huku Azam nao walibaki nafasi ya pili la pointi zao 66 kutokana na michezo 32 na watetezi Simba imebaki na alama zao 60 baada ya kushuka uwanjani mara 24, sasa hapo nani amcheke mwenzake?

HUKO mitaani kwa sasa kumekuwa na utulivu mkubwa, mashabiki wa Simba na Yanga wala hawachekani, hii ni kwa sababu timu zao zote zimepata matokeo mabaya.

Walianza Yanga walikung’utwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro, mashabiki wa Simba wakashangilia sana na kuwakejeli wenzao, lakini upeo juzi Jumamosi ukabadilika baada ya Wekundu wa Msimbazi kushtukizwa na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Wakata Miwa wa Kagera Sugar.

Ukimya umeongezeka zaidi kwa vile hata wanaoshilikia nafasi ya pili, Azam nao walikumbana na kipigo mjini Mtwara mbele ya Ndanda FC katika mechi yao na kuzifanya timu zote za nafasi tatu za juu kushindwa kuvuna alama hata moja kwa wiki iliyopita katika mechi zao za Ligi Kuu Bara.

Yanga imejikuta ikiishiwa pozi kwani wamesaliwa na alama zao 74 katika mechi 32, huku Azam nao walibaki nafasi ya pili la pointi zao 66 kutokana na michezo 32 na watetezi Simba imebaki na alama zao 60 baada ya kushuka uwanjani mara 24, sasa hapo nani amcheke mwenzake?

Achana na ishu hizo za vipigo kwa vigogo hao, unaaambiwa wakati Ligi Kuu Bara ikielekea ukingoni, tayari mabosi wa klabu kubwa nchini wakishirikiana na benchi la ufundi la timu zao wameanza mipango ya kutembeza panga la maana kuwang’oa wachezaji ambao ni watumishi hewa.

Simba na Yanga zimeanza mchakato wa kuachana na baadhi ya nyota wao waliowasajili kwa mbwembwe ili kutaka kuingia vifaa vingine vya maana kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na hususani ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya wa michuano ya Kimataifa.

Simba, Yanga na hata Azam akili zao zipo kwenye mechi za CAF kwa kuamini tiketi za ushiriki wa michuano hiyo wanaweza kuzinasa kupitia mechi za Ligi Kuu Bara na michuano ya Kombe la FA (ASFC).

Timu zote tatu bado zina nafasi ya kubeba taji la Ligi Kuu, lakini Yanga na Azam pia zina nafasi ya kunyakua tiketi ya CAF kupitia Kombe la FA kwani ni kati ya timu nne zilizokata tiketi ya nusu fainali, sambamba na Lipuli na KMC ambazo zimewashangaza mashabiki wengi wa soka kufika hatua hiyo.

Mchongo mzima upo hivi. Klabu hizo kwa kutambua kuwa michuano ya kimataifa kwa msimu ujao itatimua vumbi kuanzia Agosti, ikiwa ni wiki chache ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu wa 2019-2020, klabu hizo zimeanza mipano ya usajili mpya kwa kuanza kuzungumza na nyota mbalimbali.

Lakini hapo hapo wakipiga hesabu za kuwatema baadhi ya wachezaji ambao kwa sababu mbalimbali ikiwamo kushuka viwango.

MAJEMBE MAPYA

Mwanaspoti limenasa za chinichini kwamba kuna mazungumzo ambayo yanaendelea Jangwani kwa baadhi ya vigogo wa klabu hiyo dhidi ya majembe ya hatari kutoka nje ya nchi akiwamo straika mwenye njaa ya mabao, Roderick Mutama anayekipiga FC Lupopo ya DR Congo.

Inaelezwa Yanga inamtaka nyota huyo wa zamani wa Dynamos ya Zimbabwe ili kumuongezea nguvu Heritier Makambo, lakini katikati ya kuletwa huyo kuna nyota wanaocheza kwa sasa na Makambo ni lazima watemwe akiwamo Amissi Tambwe anayemaliza mkataba wake.

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera katika dirisha dogo lililopita la msimu huu alishaweka nia ya dhati kuwataka Umaru Kasumba wa Sofapaka na kipa Farouk Shikalo wote kutoka Kenya, lakini pia alikuwa amemleta winga Ruben Bomba kutoka DR Congo ingawa alishindwa kusaini mkataba.

Pia alimnyatia kwa karibu straika wa zamani wa Mwadui anayekipiga kwa sasa KMC, Charles Ilanfya ambaye nae walishindwa kumsajili nyota huyo kujiunga kwa Watoto wa Kinondoni.

Taarifa kutoka Yanga zinasema bado kocha anawapigia hesabu baadhi ya nyota aliowakosa dirisha dogo na kutaka kuongeza wakali wengine akiwamo Mfungaji wa bao la Mtibwa, Riffat Khamis, lakini ni lazima apige panga la maana Jangwani ili kutoa nafasi kwa wachezaji hao kutua kikosini.

Wachezaji wanaotajwa wapo kwenye hatari ya kupitiwa na panga hilo ni Tambwe, Thabani Kamusoko na Buruan Akilimali ambaye tangu amesajiliwa na kikosi hiko amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya muda mrefu. Pia kuna kina Juma Said Makapu, Kipa Beno Kakolanya.

MSIMBAZI NAKO

Katika mchakato huo wa usajili kule Msimbazi inaelezwa baadhi ya wachezaji nyota wapo njiani kuachana na klabu hiyo kutokana na mikataba yao kuelekea ukingoni, huku Emmanuel Okwi ikielezwa ameanza kuaga kabisa kuondoka Msimbazi.

Wengine wanaotajwa huenda wakakumbwa na panga ni beki Zana Coulibaly aliyesajiliwa dirisha dogo, makipa Said Mohammed ‘Nduda’ aliyepo Ndanda kwa mkopo, Deo Munishi ‘Dida’ ambao nafasi zao inaelezwa huenda ikazibwa na Kakolanya wa Yanga na kipa wa Prisons, Aaron Kalambo.

Said Ndemla, Mohammed Ibrahim, Adam Salamba, Mohammed Rashid anayecheza kwa mkopo KMC ni baadhi ya wanaotajwa kupewa mkono wa kwaheri sana na itakavyokuwa kwa Haruna Niyonzima.

Nyota wanaotajwa kupigiwa hesabu Msimbazi ili kufunika mashimo yatakayoachwa kwa wale ambao watatimka kikosini ni pamoja na Salim Aiyee wa Mwadui, George William wa Biashara United, huku ikilezwa wapo hatua ya mwishio kumrejesha Ibrahim Ajibu kutoka Yanga na kumnyakua Obrey Chirwa wa Azam, sambamba na kutajwa nyota wengine watatu kutoka nje ya nchi ambao hata hivyo majina yao yamefichwa wakisubiri kujua hatma ya Kocha Patrick Aussems kama ataongezwa mkataba ama la.

Aussems alisaini mkataba wa mwaka mmoja Julai mwaka jana kuchukua nafasi ya Mfaransa Pierre Lechantre aliyewapa taji la Ligi Kuu Bara msimu uliopita na mkataba wa Mbelgiji huyo unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu na tayari mazungumzo baina yake na Simba imeanza.

WASIKIE WADAU

Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema kikosi cha Yanga kinatakiwa kufumuliwa katika maeneo mengi ili kuunda timu ambayo unaweza kusema mpya na ikaleta ushinda msimu ujao kuliko ambavyo inacheza msimu huu.

Mwaisabula alisema Yanga kwanza haina kikosi cha kwanza ambacho kinacheza mara kwa mara muda wote wachezaji wamekuwa wakibadilika na kupishana wakati katika soka haswa mkiwa kwenye mashindano kikosi cha kwanza huwa akibadilishwa labda itokee mabadiliko ya kiufundi.

ISHU IPO SIMBA

Mwaisabula anasema mchezaji yeyote anayecheza Tanzania ambaye atasajiliwa na Simba anatakiwa kufahamu anakwenda katika timu yenye ushindani na anapaswa kuwania nafasi ya kucheza na si anafika hapo akabweteka kama walivyofanya wengine.

Alisema kwa alivyokiona kikosi cha Simba kinatakiwa kutafuta mawinga wawili kwa hapa ndani kama Dickson Ambundo kutoka Timu ya Alliance.