Simba yang'oa winga Rwanda

Muktasari:

  • Winga aliyepo kwenye rada za mabosi wa Simba ni Leandre Willy Onana (23) anayekipiga Rayon Sports na kwa sasa ndiye kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Rwanda akifunga 15 na kuasisti 10 akiwa ni mmoja ya nyota wanne ambao wapo kwenye mazungumza na mabosi hao wa Simba.

MABOSI wa Simba wamepania, kwani unaambiwa tangu Jumatatu hadi jana, walikuwa bize na vikao vya kwa nyakati tofauti kupanga bajeti ya msimu ujao, kutathimini ripoti ya kocha na usajili mpya na sasa tayari wameingia sokoni wakijiandaa kumng'oa winga kutoka Ligi Kuiu ya Rwanda.

Winga aliyepo kwenye rada za mabosi wa Simba ni Leandre Willy Onana (23) anayekipiga Rayon Sports na kwa sasa ndiye kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Rwanda akifunga 15 na kuasisti 10 akiwa ni mmoja ya nyota wanne ambao wapo kwenye mazungumza na mabosi hao wa Simba.

Simba imepania kurejesha ufalme baada ya kukosa mataji katika misimu miwili mfululizo mbele ya watani wao, Yanga na katika kufanikisha hilo imeamua kuingia sokoni kusajili mastaa wapya  ambapo kocha mkuu wa kikosi hicho, Roberto Oliveira anataka mchezaji mpya kwenye kila eneo.

Uongozi wa Simba upo tayari kumtimizia kocha Mbrazili huyo mahitaji yake na sasa umeanza mazungumzo na wachezaji wanne ambao Robertinho amewapendekeza, akiwamo winga huyo raia wa Cameroon.

Mbali na winga huyo, pia kuna beki na nahodha msaidizi wa timu ya taifa ya Rwanda 'Amavubi' beki wa kati Thierry Manzi (26), ambaye kwa sasa yuko Ubelgiji kwenye mazungumzo na moja ya timu ya huko, huku Robertinho amewaambia mabosi wa Simba kuhakikisha wanaleta bongo kwani anaamini ataongeza kitu kwenye ukuta wake na anamfahamu vyema wakiwahi kufanya kazi pamoja Rayon.

Manzi ana uzoefu wa kutosha na amewahi kuwa nahodha wa APR na Rayon na kutwaa nao mataji pia amewahi kucheza Gerogia katika timu ya FC Dila pia mwaka jana alijiunga na FAR Rabat ya Morocco lakini baadae akaomba kuondoka kutokana na mambo ya kimkataba na kurejea Rwanda alipojiunga na AS Kigali.

Kwa winga Onana ana anasifika kwa kasi, chenga na stamina akiwa na mpira lakini pia ni mtaalamu wa kufunga  akitumia zaidi mguu wa kulia.
Simba ina nafasi kubwa ya kumpata Onana kutokana na kuwa mtu wa karibu zaidi a Robertinho na taarifa za kuaminika ilizonazo Mwanaspoti, wawili hao meneja wao ni mmoja.

Ukiachana na hao, kuna wachezaji wengine wawili ambao Simba tayari imewavuta Dar es Salaam kwa mazungumzo na wapo hotelini hadi sasa.

Mapema kocha Robertinho alikaririwa na Mwanaspoti kwamba anataka kuitengeneza Simba ambayo itakuwa tishio zaidi ya ilivyokuwa msimu huu ambapo iliishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kutolewa kwa penalti na watetezi Wydad Casablanca iliyotinga fainali dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Katika Ligi Kuu licha ya kumaliza nafasi ya pili, lakini ndio timu yenye mabao mengi ikifunga 66 na kuruhusu 15 tu, huku nyota wake watatu wakiongoza orodha ya waliopiga hat trick hadi sasa akiwamo nahodha John Bocco, Saido Ntibazonkiza na Jean Baleke.

Katika hatua nyingine Mwanaspoti linajua kuna wachezaji wengine wawili kutoka Ligi ya DR Congo ambao Simba tayari imewashusha Dar es Salaam na kuwafungia hotelini  wakiendelea na mazungumzo ya kuwapa mikataba  na baada ya hapo watawatambulisha.

Wakati Simba ikiendelea na usajili huo, katika hatua nyingine timu hiyo imepanga kuachana na Mohamed Ouattara, Agustine Okrah, Gadiel Michael, Beno Kakolanya, Peter Banda, Ismail Sawadogo na Habibu Kyombo.