Simba yaleta beki wa Ulaya

Muktasari:
Joseph Stanley Okumu anayekipiga klabu ya IF Elfsborg inayoshiriki Ligi Kuu ya Sweden.
Beki huyo kisiki anayekipiga timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars ni kati ya wachezaji saba ambao Simba imepanga kuwasajili kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na ile ya Mabingwa wa Afrika.
HUKO Msimbazi baadhi ya mashabiki hawakuwa na furaha baada ya kuona beki Bakar Mwamnyeto kutoka Coastal Union akienda kwa wapinzani wao Yanga, lakini kumbe mabosi wao walikuwa na mipango mingine kabisa, ambayo sasa itawatuliza roho zao baada ya kunasa beki matata anayepiga soka barani Ulaya.
Chini ya bilionea na Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Mohammed ‘Mo Dewji’, Wekundu hao wa Msimbazi wamemebakiza hatua chache tu kabla ya kumshusha beki wa kimataifa wa Kenya, Joseph Stanley Okumu anayekipiga klabu ya IF Elfsborg inayoshiriki Ligi Kuu ya Sweden.
Beki huyo kisiki anayekipiga timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars ni kati ya wachezaji saba ambao Simba imepanga kuwasajili kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na ile ya Mabingwa wa Afrika.
Mbali na Okumu, Simba imeshasajili Ibrahim Ame, David Kameta ‘Duchu’, Charles Ilanfya, huku wakitajwa kuwashusha pia Jean Vital Ourega, Chris Mugalu na Bernard Morrison anayevutana na klabu yake kwa sasa kuhusu mkataba.
Mwanaspoti lilipata taarifa za uhakika kutoka ndani ya Simba, kuwa usajili wa mabingwa hao msimu huu utahitimishwa kwa kunaswa kwa Mkenya huyo aliyezaliwa Mei 26, 1997.
Taarifa hiyo inaeleza tayari mabosi wa Simba, wakiongozwa na Mo wameanza mazungumzo na Okumu opamoja na wasaidizi wake na mambo yanakwenda freshi kabisa.
“Kama mambo yatakwenda vizuri kati yetu pamoja na wanaomsimamia Okumu, nadhani tunaweza kuwa naye msimu ujao kutokana katika timu yetu kwa sababu tuna shida na beki wa kati mwenye uzoefu na uwezo wa kucheza mipira ya juu na kwake vyote vinapatikana,” kilisema chanzo hicho ndani ya Simba.
“Nimemfuatilia Okumu kutokana na uzoefu aliokuwa nao katika ngazi ya klabu na Kenya anaweza kuongeza kitu katika timu yetu katika mashindano ya hapa ndani na yale ya kimataifa yanahitaji wachezaji wenye ukomavu na sifa ya kucheza mashindano hayo,” alisema mtoa habari huyo aliyesisitiza kutotajwa jina.
Hata hivyo, hakuna kiongozi wa Simba aliyekuwa tayari kuthibitisha taarifa hizo za ndani, kwani simu za Mkuu wa Idara ya Habari, Haji Manara, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi, Abdallah Salim ‘Try Again’ na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Senzo Mazingisa zilikuwa zikiita bila kupokelewa.
MSIKIE JULIO
Naye kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, alisema ili kufanya vizuri kwa Simba baada ya kumkosa Mwamnyeto ni lazima ilete mabeki wa kati wawili wapya ili kuweza kumpumzisha au kucheza kwa kupishana na Pascal Wawa anayeonekana kutumika kwa muda mrefu.
Julio alisema beki itakayomleta lazima mzoefu haswa katika mashindano ya kimataifa ambayo watashiriki kwa kushindana na si kushiriki kwa maana hiyo ukiangalia wasifu wa Okumu ni mtu sahihi.
“Nadhani wanatakiwa kuwa na taarifa za kutosha za Okumu kwani, wasifu si jambo pekee linalotosha kumtambua mchezaji mzuri bali benchi la ufundi wamfuatilie vya kutosha na kupata mchezaji, ambaye atacheza vizuri mfululizo si kuwa na mchezaji mwenye kiwango cha kupanda na kushuka,” alisema.
“Ukiachana na hilo la Okumu shaka yangu ipo kwa beki mwingine wa kati, Ibrahim Ame aliyesajiliwa anafaa kweli kwenda kucheza Simba au wamemchukua kama mbadala baada ya kumkosa, Mwamnyeto aliyekwenda Yanga, majibu ya haya yote tutayapata msimu ukianza,” alisema Julio.
HUYU NDIO OKUMU
Okumu alikuwa katika kikosi cha Harambee Stars kilichoshiriki Fainali za Afrika (Afcon 2019) wakipangwa kundi moja na Tanzania, akicheza sambamba na Mussa Mohammed eneo la ulinzi huku mbele kukiwa na mashine matata kama Victor Wanyama na Michael Olunga.
Katika mechi zote tatu za Afcon zilizofanyika Misri, Okumu alianza na kucheza dakika zote ikiwamo ile ya Algeria waliokuja kuwa mabingwa akiwazuia kina Riyad Mahrez anayekipiga Manchester City ya England pia hata kwenye mchezo dhidi ya Senagal alimkabili vilivyo Sadio Mane wa Liverpool.
Hata walipovaana na Tanzania, aliwabana Mbwana Samatta na Simon Msuva na kuisaidia Kenya kushinda 3-2 na mechi hiyo kutibua hesabu za Taifa Stars kwani, walipoteza mechi zao zote na kumaliza michuano hiyo bila pointi hata moja.
Okumu alianza kucheza soka la ushindani 2014-16 ndani ya Chemelil Sugar ya Kenya kabla ya 2016–17 kutimkia Free State Stars ya Afrika Kusini na baadaye kwenda AFC Ann Arbor na mwaka juzi hadi mwaka jana alikuwa Real Monarchs kabla ya kujiunga na IF Elfsborg aliyonayo mpaka sasa. Wadau wa soka la Kenya, tayari wanaamini Okumu ataungana na Francis Kahata pale Msimbazi.