Simba yakwepa figisu za Wasauzi

Simba yakwepa figisu za Wasauzi

SIMBA wajanja sana. Baada ya kushtukia huenda wakazinguliwa Afrika Kusini katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates, mabosi wameukwepa mtego huo.

Mabosi hao wameamua kuipeleka timu nchini humo siku moja kabla ya mchezo utakaochezwa mjini Johnnesburg, huku ikiwa tayari imeanza kutanguliza watu wa kuweka mazingira sawa kabla ya timu kupaa Jumamosi.

Tayari Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez yupo mitaa ya Soweto, Afrika Kusini kuweka mazingira sawa kuipokea timu na ameliambia Mwanaspoti kuwa licha yake, pia vigogo wengine watatangulia mapema, lakini kikosi kitatua Jumamosi siku moja kabla ya mechi.

“Lengo letu Afrika Kusini ni moja tu ambalo ni kupata matokeo yatakayotufanya tufuzu nusu fainali. Tayari nipo hapa na timu itawasili Jumamosi siku moja kabla ya mchezo,” alisema Barbara.

Simba imeamua kufanya hivyo ili kuepuka usumbufu ndani ya kikosi chake nchini humo na hadi sasa timu inaendelea kujifua kwenye uwanja wake wa Bunju ili imalize kila kitu huku na Kusini iende kucheza mechi.

Katika mchezo huo utakaopigwa Jumapili Aprili 24, kwenye Uwanja wa Orlando kuanzia saa 1:00 usiku, Simba itahitaji ushindi au sare ili kutinga nusu fainali jambo ambalo uongozi, benchi la ufundi na wachezaji wameapa kufa na kupona kuhakikisha linatimia.

Barbara ameweka msisitizo Simba imebadilika, inajua ugumu wa mechi ugenini lakini kila mmoja ndani ya timu yupo tayari kwa nafasi yake kuhakikisha inatinga nusu fainali. “Tunajiamani tunaenda kufanya vizuri, kocha na benchi la ufundi kwa ujumla wanaendelea na maandalizi kwa morali ya juu kuhakikisha tunapata matokeo tunayoyahitaji kwenye mchezo wa marudiano, jambo ambalo linawezekana kwani Simba imebadilika na inastahili kusonga mbele zaidi,” alisema Barbara.

Pia aliweka wazi kuhusu tuhuma za kocha wa Pirates Mandla Ncikazi, alizotoa akiishutumu Simba kuwapokea vibaya kwenye mchezo wa kwanza walipoteza bao 1-0.

“Alitaka kuichafua Simba na taifa kwa ujumla, tayari tumechukua hatua juu yake kwa kumripoti sehemu husika na tunaamini maamuzi yatafanyika kwa haki.

“Simba ni timu kubwa kwa sasa, timu nyingi zinataka kuwa kubwa kupitia Simba hivyo hatutaruhusu mtu yeyote aichafue kwani hii ni taasisi yenye watu makini na malengo makubwa,” alisema.

Mwanaspoti linajua kuwa Clatous Chama ambaye hayuko katika usajili wa kimataifa, John Bocco na Hassan Dilunga walio majeruhi na Bernard Morrison asiye na vibali vya kuingia Sauzi ndio watakosekana mechi hiyo.