Simba yakiri kosa CAF, kulipa faini

SIMBA imekiri kosa na kubainisha kuwa haina budi kulipa faini ambayo Bodi ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imewatoza.

Jana CAF ilieleza kuitoza klabu hiyo faini ya Sh23 Milioni kwa kosa la kuwasha moto eneo la katikati ya uwanja wakati wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya kusali.

Picha za tukio hilo zilisambaa wakati wa mchezo wa marudiano wa robo fainali ya CAF nchini Afrika Kusini, Simba ilipocheza na wenyeji, Orlando Pirates.

Katika mchezo huo, Simba ilifungwa bao 1-0 na kuondoshwa kwa mikwaju ya penalti kufuatia ushindi wa bao 1-0  ilioupata awali nyumbani kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huku wenyeji wakitinga nusu fainali.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally amesema hawana cha kujitetea kwenye adhabu hiyo, ni kosa walifanya hivyo hawnaa budi kulipa faini hiyo.

'Taarifa za adhabu hiyo tunazo na hatuna budi kulipa faini kwa kuwa ni kosa ambalo limeshafanyika na CAF imetoa adhabu yake," alisema Ahmed.

Alipoulizwa sababu za wao kuwasha moto uwanjani, alisema hayo si ya kuzungumza kwa kuwa yalishatokea na CAF imewaadhibu kwa kosa hilo.

Awali, gazeti hili lilimtafuta Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu ambaye aliomba atafutwe Ahmed au Ofisa Mtendaji mkuu wa klabu, Barbara Gonzalez.

"Mtafute Barbara au Ahmed watakujibu, kwa sasa siko kwenye nafasi ya kuzungumzia hilo," amesema Mangungu kwa kifupi kabla ya Ahmed kubainisha kwamba wameipokea adhabu na hawana budi kulipa faini.

Hata hivyo CAF imetoa mwanya wa Simba kukata rufaa siku tatu baada ya hiyo iliyotolewa Mei 15, ambayo mwisho wa rufaa hiyo ni kesho.