Simba yaishusha Azam, Chama atupia mbili

SIMBA leo imepanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya  imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa, huku kiungo Mzambia Clatous Chama akitupia yote mawili.

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam, ulikuwa wa 19 kwa Simba na 21 kwa Mashujaa na kufanya Simba ikae nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi 45 nyuma ya kinara Yanga yenye 52, huku Mashujaa ikishuka hadi nafasi ya 12 na pointi zake 21.

Mchezo huo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa nyakati tofauti, lakini kadri muda ulivyoenda Simba ilizidi kutawala mchezo na dakika 45 za kwanza zikamalizika kwa suluhu.

Simba ilirejea kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ikimtoa Freddy Michael na kuingia Willy Onana aliyechangamsha mchezo.

Dakika ya 57 Simba iliandika bao la kwanza kupitia kwa Chama aliyefunga kitaalamu akimalizia pasi ya Onana.

Dakika ya 73 Chama aliifungia Simba bao la pili baada ya kupokea pasi ya Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr'.

Mabao hayo yamemfanya Chama kufikisha mabao sita huku asisti ya 'Zimbwe Jr' ikiwa ya nne kwake.

Wakati mchezo ukiendelea Mashujaa ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Idrissa Stambuli, David Ulomi na Ibrahim Ame na nafasi zao kujazwa na Mapinduzi Balama, Baraka Mtui na Emmanuel na baadae kutoka Omary Adam na Adam Adam ambao nafasi zao zilichukuliwa na Hassan Haji sambamba na Abdul Nasr.

Kwa upande wa Simba walitoka Kibu Denis, Babacar Sarr, Henock Inonga, Freddy na Chama na nafasi zao kuzibwa na Mzamiru Yassin, Luis Miquissone, Keneddy Juma na Pa Omar Jobe.