Simba yaenda mapumziko kifua mbele

SIMBA imemaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza cha mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar ikiongoza kwa mabao 2-0 katika mchezo unaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mchezo huo Simba inaoutumia kumuaga beki wake Pascal Wawa aliyemaliza mkataba wake baada ya kudumu na Wekundu wa Msimbazi hao kwa misimu minne ilianza kwa kasi huku timu zote mbili zikishambuliana kwa zamu.

Katika dakika 15 za mwanzo timu zote zilishambuliana kwa kupokezana lakini umakini katika kumalizia nafasi kwa washambuliaji Kibu Denis (Simba) na Bryan Mayanja wa Mtibwa ulikuwa mbovu.

Mtibwa iliendelea kulishambulia lango la Simba bila mafanikio na dakika ya 17 Simba ilipata bao la kuongoza kupitia kwa Pape Sakho.

Sakho alifunga bao hilo la sita kwake msimu huu kwenye ligi baada ya kukokota mpira na kumpa pasi Kibu Denis aliyemrudishia kwenye njia na kufunga.

Mchezo uliendelea kwa timu zote kumiliki mpira kwa kupokezana huku pasi fupi fupi zikipigwa hususani katikati ya uwanja lakini hazikubadili matoke.

Dakika ya 44 kipa wa Mtibwa Shaban Kado alijifunga baada ya Peter Banda wa Simba kupiga shuti lilioenda golini na kipa huyo kuutema kisha kudakia ndani.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika ubao wa matokeo ulikuwa ukisomeka Simba 2-0 Mtibwa Sugar.