Prime
Simba yaanza kufyeka hawa

Muktasari:
- Simba inashika nafasi ya pili kwa sasa katika msimamo ikiwa na pointi 71, moja pungufu na ilizonazo Yanga inayoongoza na kila moja ikisaliwa na mechi tatu ikiwamo kiporo cha Dabi ya Kariakoo iliyoahirishwa Machi 8 na kupangwa kupigwa Juni 15.
MASHABIKI wa Simba wanaendelea kuchekelea ushindi wa 23 kwa msimu huu katika Ligi Kuu kwa kuilaza Singida Black Stars, lakini mabosi wa klabu hiyo wameanza kufanya maboresho ya kikosi hicho kimya kimya, ikiwemo kujiandaa kutembeza panga kwa baadhi ya mastaa na kuleta majembe mapya.
Simba inashika nafasi ya pili kwa sasa katika msimamo ikiwa na pointi 71, moja pungufu na ilizonazo Yanga inayoongoza na kila moja ikisaliwa na mechi tatu ikiwamo kiporo cha Dabi ya Kariakoo iliyoahirishwa Machi 8 na kupangwa kupigwa Juni 15.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa, kuna majina ya nyota kadhaa yatakayofyekwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kumalizika kwa mikataba na pia kushindwa kupata namba kikosini na tayari watakaochukua nafasi zao, wameanza kufanyiwa mazungumzo kuweka mambo sawa watue.
Kati ya majina yanayotajwa huenda yakafyekwa ni beki wa kati Hussein Kazi anayemaliza mkataba, kipa Hussein Abel, winga Edwin Balua (kakosa namba), Aishi Manula (mkataba unaisha), Valentino Mashaka (kakosa namba) Augustine Okejepha.
Tayari kuna tetesi kuhusiana na Manula kuhusishwa na Yanga na Azam, kutokana na kukosa nafasi ya kucheza Simba, mechi yake ya mwisho ilikuwa dhidi ya Tanzania Prisons iliyowafunga 2-1 mjini Morogoro baada ya awali kukubali kichapo cha 5-1 katika Dabi ya Kariakoo Novemba 5, 2023.
“Kuna majina yameshawekwa katika orodha ya kufyekwa kutokana na sababu mbalimbali kwa mujibu wa mapendekezo ya kocha, lakini kuna wengine wanaopigiwa hesabu za kuletwa kikosini,” kilisema chanzo hicho.
Ukiachana na hao, majina yanayotajwa kufanya mazungumzo na klabu hiyo ni kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayeongoza kwa asisti 13 na mabao manne, beki anayemaliza mkataba Coastal Union, Lameck Lawi, Gibril Sillah wa Azam anayemiliki mabao tisa ya Ligi Kuu, hao ni baadhi tu.
Mwanaspoti lilimtafuta Kazi, kuthibitisha taarifa hizo, alisema ni kweli mkataba wake unaishia msimu huu na bado hawajaanza mazungumzo na viongozi kuhusu mkataba mpya, hivyo anaamini lolote linaweza likatokea.
“Nipo 50 kwa 50 inawezakana kuachwa ama kusalia, kwani ni maisha ya kawaida kwa mchezaji ama makocha leo unamkuta timu hii kesho ile, kikubwa ni kutokukata tamaa kupambana mpira wa miguu ni kazi yangu,” alisema Kazi ambaye kacheza dakika 10 tu dhidi ya KMC na kuongeza;
“Ninachojivunia sitaondoka bure Simba, nimepata medali ya CAF ambayo imetafsiri kitu kikubwa katika CV yangu ya soka, ila ukweli mkataba wangu unaisha na bado sijazungumza chochote na viongozi.”
Tangu Kazi ajiunge na Simba msimu uliyopita akitokea Geita Gold, hajawa na nafasi kubwa ya kucheza mbele Che Malone, Abdulrazak Hamza aliyokiri ni wachezaji wazuri na wanatumia vyema nafasi wanazopata.
“Kwa wazawa Hamza ni beki mzuri, anatumia akili na mwepesi wa kung’amua hatari zinapokuja mbele yake, anazitumia vizuri nafasi anazopata za kucheza,” alisema Kazi ambaye kwa mara ya kwanza aliichezea Simba B 2015.