Simba wapewa mbinu za dakika 5, Mzimbabwe atoka kambini Platinum

MAKOCHA wawili wenye heshima kubwa ndani ya Simba,wamewasisitiza wachezaji wa klabu hiyo kupata bao la haraka ndani ya dakika tano za kwanza kwenye mchezo wa kesho Jumatano dhidi ya FC Platinum.
Lakini huko kambini Platinum,wanamuwaza Calvin Mavhunga ambaye ni mtaalam wa Zimbabwe aliyewachomoka na sasa yuko Simba akiwapa mbinu za kuumaliza mchezo huo. Kinachowauma Platinum ni kwamba Mavhunga anajua mambo yao mengi ya ndani kwavile alikuwa nao kambini na mazoezini wakati wanajiandaa na mechi ya awali ya Simba. Lakini vilevile aliwahi kuwasaidia Orlando Pirates kuusoma mchezo na kuucheza hivyohivyo wakawatoa nishai Platinum mwaka jana katika hatua ya makundi.
Makocha wazawa,Salum Madadi na Abdallah Kibadeni wameiangalia Simba na kuwaambia kwamba wanauwezo wa kuishinda mechi hiyo kirahisi zaidi hata kabla giza halijaingia kwani mechi inaanza rasmi saa 11 jioni.
Madadi amesema; “Kwanza ni kurekebisha makosa ya mechi iliyopita, pia makocha watakuwa wameona ubora na udhaifu wa wapinzani hivyo katika maeneo hayo wanapaswa kuongeza nguvu zaidi.
“Ila kikubwa wachezaji wawe watulivu, Simba ina wachezaji wenye uwezo wa kupambana na kushinda, hivyo wacheze kama majukumu ya
kushambulia na kuzuia yawe ya wote, wacheze pamoja,” alisema Madadi na kuwataka Simba wapate bao la kuongoza hata dakika ya kwanza ya mchezo ili liwasaidie kuwatoa mchezoni Platinum na kuwapa nguvu mashabiki ndani ya Uwanja wa Mkapa.Amewasisitiza kujifua kwa nguvu kimbinu kuhakikisha wanaanza vizuri mechi hiyo.

Kibadeni amewataka Simba kama itaweza ndani ya dakika tano ipate bao la kuongoza kuumiliki mchezo huo. “Hii itawavuruga wapinzani, lakini pia itawaongezea morali Simba, pia wachezaji wajiongeze wakapambane, Platinum ina wachezaji wenye nguvu na wanacheza kitimu ila nyumbani ni nyumbani tu, wachezaji wetu watulie na watekeleze kile kocha atakachowambia, ushindi kwa Simba upo,” alisema Kibadeni kocha wa zamani wa timu hiyo.
Kuhusu Calvin kuimaliza Platinum ajira yake imewavuruga Wazimbabwe. Kazi ambayo Simba imempa ni kuusoma mchezo wa Platinum na kuwapa benchi la ufundi mbinu mbadala.Mtaalam ni kiongozi pia wa chama cha soka cha Zimbabwe jambo ambalo limefanya raia wenzie wamshambulie kwa maneno mitandaoni wakidai hana uzalendo na ameigeuka nchi yake kwa maana ya Platinum. Simba inahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kusonga mbele baada ya kupoteza bao 1-0 ugenini. Platinum ambao wamekuja na kikosi chote wapo Jijini Dar es Salaam wakijivunia rekodi ya kufuzu hatua ya makundi misimu yote miwili iliyopita.
Kwa mujibu wa Haji Manara, Simba imepania kufuzu hatua ya makundi ya Afrika kwa mara nyingine huku akisisitiza kwamba kauli yao ni ileile ; “War in Dar” wakimaanisha ni vita ndani ya Dar.