Simba waja na Tik-Tak kwa Mkapa

Simba waja na Tik-Tak kwa Mkapa

Muktasari:

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Jumapili iliyopita nchini Nigeria Simba ilianza vizuri mashindano hayo kwa kupata uhsindi wa bao 1-0 dhidi ya Plateau United.

KULEKEA mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya mwenyeji Simba na Plateau United ya Nigeria wekundu msimbazi wamekuja na kauli mbiu iitwayo Tik-tak kwa Mkapa.


Kauli hiyo imetambulishwa rasmi leo Jumatano na Ofisa habari wa Simba,Haji Manara kwenye mkutano na waandishi wa habari ambapo aliambatana na mwenyekiti wa timu hiyo Mwina Kaduguda.


Simba itaikaribisha Plateau United Jumamosi katika mchezo wa marudiano utakaoanza saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Manara ameeleza sababu za kuja na kauli hiyo  
“Sisi ndio wataalamu, tuna kauli zetu zinazotupa hamasa na nguvu kwenye michezo hii, sasa kwakua ndio mara ya kwanza kucheza mchezo wa kimataifa kwa ngazi ya klabu toka ametangulia mbele za haki aliyetujengea uwanja ambao tutauchezea mechi hiyo basi kauli ya Tik-Tak (Tikitaka) kwa Mkapa itatufaa zaidi ikiwa ni pamoja na kumuenzi mzee wetu Hayati Benjamin Mkapa,” amesema Manara.


Sambamba na hilo Manara ametoa ufafanuzi juu ya mashabiki watakaoruhusiwa kuingia uwanjani Jumamosi kuwa ni wale tu watakaovaa jezi za Simba huku pia akiwataka kuwa wazalendo.
“Hili ni suala la kitaifa, mashabiki mnapaswa kuja kuishangilia Simba kwa uzalendo mkubwa maana tukishinda sisi basi Tanzania nzima imeshinda hivyo tunawakaribisha sana lakini natoa tahadhari kuwa mashabiki wanapaswa kuvaa jezi za Simba pekee, sidhani kama tutaruhusu waliovaa jezi za wapinzani kuingia uwanjani,” alisema Manara.


Pia mwenyekiti wa klabu ya Simba, Mwina Kaduguda, amewashukuru wadau, wachezaji, na watanzania wote kwa kuonesha sapoti katika  mchezo wa kwanza uliofanyikaJumapili iliyopita nchini Nigeria.


“Ninawashukuru wachezaji wote wa Simba kwa kupeperusha vyema bendera ya timu yetu na Tanzania kwa ujumla kwani wametuwakilisha vyema huko nchini Nigeria walikocheza na kushinda mchezo wa kwanza dhidi ya Plateau United,”.

“Plateau ni timu kubwa kama ilivyo Nkana FC ya Zambia ama AS Vita ya Congo hivyo wachezaji, wadau na mashabiki wa Simba  wasiibeze kikubwa tuombe dua tushinde mchezo wetu wa marudiano Jumamosi pale kwa Mkapa kisha tusonge mbele,” amesema Kaduguda.