Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba wafanyie kazi hapa...

BAADA ya kupoteza ugenini dhidi Asec Mimosas huko Benin kwa mabao 3-0, wawakilishi wa Afrika Mashariki na Kati kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Simba wanahitaji ushindi tu katika mechi ya mwisho dhidi ya USGN ili watinge robo fainali.

Mchezo huo wa mwisho utachezwa Aprili 3 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika kundi D, Asec ndio vinara wakiwa na pointi tisa, RS Berkane wa pili na pointi zao saba sawa na Simba iliyo ya tatu huku USGN wakiwa wa mwisho na pointi tano.

Kama Simba watafungwa na USGN wataondolewa katika mashindano na wakitoka sare wataiweka nafasi ya kusonga mbele hatarini kwani Berkane na Asec wanaweza kufuzu wenyewe.

Ifuatayo ni orodha ya kasoro ambazo Simba inapaswa kuzishughulikia ili ifanye vyema:


MABAO YA KROSI

Kwenye misimu mitano mfululizo katika mashindano ya kimataifa na yale ya ndani Simba wamekuwa wakifungwa mara kwa mara mabao yatokanayo na krosi.

Msimu huu Simba wamefungwa na Berkane, Red Arrows na Asec kama ilivyokuwa pia na Jwaneng Galaxy. Kutokana na mifano hiyo ili wamalize mechi ya mwisho salama bila ya kuruhusu bao wanapaswa kushughulikia hilo.


NIDHAMU

Katika mechi ya nyumbani Simba wanatakiwa kucheza kwa nidhamu kubwa ili kushinda na wachezaji kutopata kadi nyingi za njano kama ilivyokuwa michezo iliyopita.

Mechi iliyopita dhidi ya Asec wachezaji wengi walishindwa kucheza kwa nidhamu na kuna waliostahili hata kadi nyekundu. Katika mchezo huo Simba waliopewa kadi za njano walikuwa Aishi Manula, Meddie Kagere, Taddeo Lwanga na Pascal Wawa kutokana na kucheza faulo jambo wanalotakiwa kulitibu.

Kama watapata kadi za njano nyingi inaweza kutokea mmojawao akapata nyekundu au wengine kushindwa kucheza robo fainali iwapo watafuzu kutokana na kupata kadi nyingi.

Takwimu zinaonyesha katika mechi tano za makundi Simba wameonyeshwa kadi za njano 14.


KUKOSA MABAO

Miongoni mwa shida zinazowasumbua Simba msimu huu wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini kati ya hizo zinatumika chache au kutotumika vizuri.

Miongoni mwa sababu inayochangia Simba kutofunga mabao mengi ni kushindwa kufanya vizuri kwa mastraika Chriss Mugalu, John Bocco na Meddie Kagere. Msimu uliopita watatu hao walikuwa hatari kufunga mabao ikiwemo yale muhimu pengine ndio maana walikuwa na safu kali ya ushambuliaji katika mashindano mbalimbali.

Katika ligi msimu uliopita Bocco alimaliza kinara akiwa na mabao 16, Mugalu wa pili (15) wakati Kagere alikuwa na 14 na walifunga hata Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kama Simba wataendelea na shida ya kukosa mabao katika mchezo na USGNwatapitia wakati mgumu wa kupata ushindi ikiwezekana ule wa mapema na kupunguza presha dakika za mwisho.


USGN TANO

Ukiangalia msimamo wa kundi D utagundua USGN wanacheza mechi hiyo wakihitaji ushindi na si matokeo mengine kwani wakifanikiwa kufanya hivyo wanaweza kusonga robo fainali.

Kutokana na hilo ni wazi mchezo utakuwa mgumu. USGN katika mechi tano walizocheza tatu nyumbani na mbili ugenini hakuna hata moja waliyomaliza dakika 90 bila kufunga bao.

Kucheza mechi tano bila kufunga bao Simba wanatakiwa kuwa na tahadhari kubwa dhidi yao kwani wasipokuwa makini wageni wanaweza kuendeleza rekodi ya kufunga michezo yote hatua ya makundi.

Simba wanapokuwa nyumbani ni wazuri katika kushambulia kutokana na kuhitaji ushindi zaidi, ila kuna nyakati wamekuwa wakifanya makosa ya kiulinzi mpaka wapinzani wao kutumia kufunga mabao.


KUJIAMINI KUPITILIZA

Wachezaji wa Simba pamoja na baadhi ya mashabiki wanaweza kuingia katika mechi hiyo wakiwa na uhakika wa kuwafunga USGN kutokana na mambo mawili makubwa.

Kwanza, mwendelezo wa matokeo mazuri nyumbani pamoja na sare ya bao 1-1 walipocheza na timu hiyo katika mchezo wa mzunguko wa kwanza nchini Niger.

Kama wataingia na mambo hayo wanaweza kushangazwa kwa kufungwa kama ilivyokuwa mechi na Jwaneng Galaxy jambo ambalo halikutegemewa wengi.

Simba katika mechi hiyo walijiamini baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 ugenini na dakika 45 za kwanza walikuwa mbele kwa bao 1-0 nyumbani, ila mwisho wa siku walifungwa 3-1,na kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kama Simba walipata sare ugenini hata USGN nao wanaweza kufanya hivyo kutokana nao kutafuta nafasi ya kufuzu robo fainali.


WASIKIE WADAU

Mchezaji wa zamani wa Taifa Stars, Amri Kiemba anasema Simba hawatakiwi kucheza mechi hiyo kwa ulaini. “Miongoni mwa mechi Simba wanayotakiwa kucheza kwa nidhamu kubwa katika kuzuia na kushambulia ni hii kwani wakifanya makosa kutokana na USGN walivyo bora kwenye maeneo mengi wanaweza kuwafunga,” anasema Kiemba.

Kocha wa zamani wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi alisema Simba wamekuwa na shida ya kuzuia na kucheza kwa mazoea ndio maana wamekuwa wakifungwa mabao yanayotokana na krosi mara kwa mara.