Kisa Yanga, maafande Tanzania Prisons waitana fasta

Muktasari:
- Josiah alisema kwa mechi walizocheza mfululizo, vijana wameonesha utulivu wakipata matokeo yenye kutia matumaini, hivyo michezo iliyobaki ni kufa na kupona.
Wakati Tanzania Prisons ikiingia kambini leo Jumapili kuendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi zilizobaki kukwepa presha ya play off, viongozi wameamua kuitana haraka kuimaliza Yanga.
Maafande hao hawapo sehemu nzuri wakiwa na pointi 30 katika nafasi ya 13, wanatarajia kushuka uwanjani Juni 18 kuikaribisha Yanga yenye pointi 73 na inayohitaji ushindi kujiweka pazuri kutetea taji kwa msimu wa nne mfululizo, lakini Prisons ikitaka kuiokoa kuangukia katika play off.
Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, John Matei amesema wakati wachezaji wakirudi kambini, uongozi unatarajia kuitana katika kikao cha dharura, ambapo pamoja na mambo mengine watajadili namna ya kupata pointi tatu dhidi ya Yanga.
Matei alisema uongozi unafahamu uzito na umuhimu wa mechi mbili zilizobaki wakianza na Yanga kisha kumaliza msimu dhidi ya Singida Black Stars, hivyo inahitaji mipango ya haraka ili kufikia malengo.
“Kwa sasa ni mapema kuweka wazi mipango yetu hicho kikao cha dharura, lakini tutakapokutana tutakuja na maazimio, kumbuka tuna mechi ngumu na muhimu mbeleni,” amesema Matei.
Kwa upande wa kocha mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah alisema kwa kuwa hajawahi kuwa na historia ya kushusha timu, anahitaji kuendelea na heshima hiyo, akituliza mashabiki kuwa Prisons lazima ibaki Ligi Kuu.
Josiah alisema kwa mechi walizocheza mfululizo, vijana wameonesha utulivu wakipata matokeo yenye kutia matumaini, hivyo michezo iliyobaki ni kufa na kupona.
“Lazima tucheze kwa nidhamu na utulivu, tunajua mechi zilizobaki si nyepesi, hatupaswi kuangalia tunacheza na nani au wapi badala yake tubaki kwenye malengo yetu,” amesema kocha huyo.