Simba Queens nayo ina historia tamu

LEO Jumatatu ni siku muhimu kwa mashabiki, wapenzi na wanachama wa Simba ambao huadhimisha tamasha lao lijulikanalo kama ‘Simba Day’, tofauti na 2014 lilipofanyika Agosti 9.

Tamasha hilo lilianza rasmi 2009 chini ya mwenyekiti wa wakati huo, Hassan Dalali pamoja na katibu wake Mwina Kaduguda kwa lengo la kuwakutanisha viongozi, wanachama, wachezaji na mashabiki huku likitawaliwa na wasanii mbalimbali.

Ndani ya klabu hiyo, pia timu ya wanawake inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka la Wanawake (WPL) ambayo Simba Queens imefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo mara tatu.

Makala haya inakuletea historia fupi ya namna Simba Queens ilivyopata mafanikio wakati huu ikielekea kilele cha tamasha hilo.


MWAKA ILIOAZISHWA

Timu hiyo ilianzishwa 2016 kisha msimu wa 2017/18 ikaanza kushiriki rasmi Ligi Kuu ya Wanawake (Serengeti Lite Women’s Primier League).

Kwa mara ya kwanza Ligi ya Wanawake hapa Tanzania ilianza kuchezwa msimu wa 2016/17, ambao bingwa wa kwanza ni Mlandizi Queens, ambayo ndio ilikata utepe na kuandika historia ya michuano hii ambayo imeanza kuwa gumzo nchini.

Baada ya hapo kijiti cha ubingwa kilitua JKT Queens, ambao ilishinda kombe hilo mara mbili mfululizo kuanzia msimu wa 2017/18 na 2018/19.


YAVUNJA REKODI

Baada ya JKT Queens kushinda mara mbili mfululizo rekodi ilikuja kuvunjwa na Simba Queens iliyoshinda mara tatu mfululizo kuanzia msimu wa 2019/20, 2020/21 na 2021/22.


MGOSI NOMA

Katika mataji hayo matatu, mawili yalichukuliwa na kocha aliyewahi kukinoa kikosi hicho, Mussa Hassan Mgosi msimu wa 2019/20, 2020/21.

Taji moja la msimu ulioisha wa 2021/22 lilichukuliwa na Sebastian Nkoma aliyeanza kuifundisha Novemba Mosi 2021 akichukua nafasi ya Hababuu Ally.


TUZO TANO

Katika hafla ya Tuzo za Shirikisho la Sooka Tanzania (TFF) zilizotolewa Julai 7, mwaka huu timu hii ilishinda tano ambazo ni kocha bora iliyochukuliwa na Nkoma, Ubingwa, Mfungaji Bora iliyoenda kwa Asha Djafar akifunga mabao 27 wakati Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ akichukua Tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu (MVP) huku Gelwa Yona akichaguliwa kuwa kipa bora.


MSIKIE MGOSI

Mgosi anasema lengo ya kuanzishwa kwa timu hiyo ni kufuata nyayo za kaka zao (Simba); “Kwa timu ya wanaume tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa hivyo tulitaka pia na kwa wanawake tupige hatua jambo ambalo limefanikiwa.”


SIMBA B

Unapotaja soka la vijana kwa upande wa klabu za Ligi Kuu Bara, huwezi kuiacha Simba, kutokana na mafanikio makubwa waliyoyapata kwa maana ya makombe mbalimbali walivyobeba na pia uzalishaji wa vipaji vinavyotamba katika timu mbalimbali hadi sasa.


ILIOANZISHWA 2008

Ilianzishwa rasmi 2008 baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa masharti kwa kila klabu inayoshiriki Ligi Kuu Bara kuwa na timu za vijana.


KOCHA WA KWANZA

Baada ya kuanzishwa kwa timu hiyo, kocha wa kwanza kuifundisha ni Issa Masharubu na mwaka mmoja mbele yaani 2009 ikawa chini ya aliyekuwa Rais wa Simba, Evans Aveva, Katibu Mulamu Ng’ambi ambaye ni (Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi) na Kassim Dewji.


MASHINDANO YA KWANZA

Mashindano ya kwanza kushiriki kikosi hicho ni Kombe la Uhai na kufika fainali ambayo ilipoteza kwa kufungwa mabao 3-2 na Azam ‘B’.


WACHEZAJI WA MWANZONI

Baadhi ya nyota ambao walikuwa kwenye kikosi hicho mwanzoni wakati kinaanzishwa ni, Godfrey Wambura aliyekuwa nahodha wa timu, Hamad Kibacha, Faraji Kabali, Rajab Zahiri na Kelvin Charles.


TAJI LA KWANZA

Kombe la Rollingstone ndilo la kwanza kubebwa na kikosi hicho kwenye mashindano yaliyofanyika Jijini Arusha na ilikuwa mwaka 2009.

Mbali na taji hilo, vijana hao walichukua tena mataji mengine yanayotambulika yakiwemo, Kinesi, Uhai na Bank ABC.

Katika kikosi kilichochukua ubingwa wa Bank ABC kiliundwa na baadhi ya wachezaji kina Abuu Hasheem, Wiliam Lucian ‘Galas’, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Abdallah Seseme, Kenny Ally, Haroun Chanongo, Ramadhani Singano (Messi) na Miraji Adam ambao wanacheza sehemu mbalimbali.


MFUMO ULIOTUMIKA

Ili kupata vijana ambao wanakidhi kuichezea timu hiyo ilitumika vyombo mbalimbali vya habari kama magazeti na redio ili kutangaza kuhusu majaribio ya wanaoweza kucheza soka.


CHANGAMOTO

Timu hii ila ilipitia changamoto ikiwemo hali mbaya ya kifedha kwani ilikuwa ikiendeshwa kwa pesa za wadau kipindi hicho hakuna bajeti rasmi iliyotengwa kwenye soka la vijana.


MSIKIE RWEYEMAMU

Aliyekuwa meneja wa kikosi hicho, Patrick Rweyemamu anasema siri ya mafanikio wakati wao ni ushirikiano baina ya uongozi wa Mzee Dalali, benchi la ufundi na wadau hasa kundi kubwa lililokuwa na ushawishi la ‘Friends Of Simba’.