Simba, Namungo washikilia ratiba ya Mapinduzi Cup

Muktasari:
WAWAKILISHI wa michuano ya kimataifa nchini, Simba na Namungo FC ndiyo wameshikilia upangaji wa ratiba ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi, ingawa tayari zimethibitisha ushiriki wao.
WAWAKILISHI wa michuano ya kimataifa nchini, Simba na Namungo FC ndiyo wameshikilia upangaji wa ratiba ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi, ingawa tayari zimethibitisha ushiriki wao.
Mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka visiwani Zanzibar yanatarajiwa kuanza Januari yakishirikisha timu tisa ambapo tano zinatoka Bara na nne ni za Zanzibar.
Mashindano hayo ni maalumu kwa ajili ya sherehe za kuazimisha siku ya mapinduzi ambapo Simba na Namungo zinashiriki michuano ya kimataifa ya Afrika.
Leo Jumatano, Simba na Namungo zitakuwa na mechi ambapo Simba inacheza na FC Platinum jijini Harare mechi ya Ligi ya Mabingwa wakati Namungo ipo nyumbani ikiikaribisha El Hilal ya Sudan ikiwa ni mechi ya Kombe la Shirikisho
Afrika, huku mechi za marudiano zitachezwa kati ya Januari 5 na 6, mwakani.
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Unguja, Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano hayo, Khamis Said alisema walituma barua kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya timu za Bara na tayari wamejibiwa kwa mdomo kukubali kushiriki wa timu hizo.
“Ratiba haijapangwa, ila timu zote za Bara zimethibitisha kushiriki japo tunasubiri uthibitisho wao wa maandishi na tumewapa muda hadi Desemba 25, tunatambua kazi ngumu waliyonayo Simba na Namungo lakini tunaamini watashiriki,” alisema Said.
“Ikumbukwe kuna mwaka Simba walikuwa na majukumu ya kimataifa, lakini walituma wachezaji wengine ambao walibaki na kikosi kingine kilijiunga baadaye, hivyo hilo linajulikana hatudhani kama watakuwa tofauti.
“Kwenye michuano hii uwepo wa Simba na Yanga unaleta hamasa na ushindani mkubwa kutokana na historia zao kwenye soka.”
Mbali na Simba, Namungo na Yanga timu zingine kutoka Bara ni Azam na mabingwa watetezi wa kombe hilo, Mtibwa Sugar.