Simba mzuka mwingi... Yaweka mikakati mizito Botswana

Muktasari:

SIMBA wanataka kuanza kwa kasi na kumaliza kabisa mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy watakapokutana Jumapili hii nchini Botswana.

SIMBA wanataka kuanza kwa kasi na kumaliza kabisa mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy watakapokutana Jumapili hii nchini Botswana.

Na hilo linatokana na Kumbukumbu ya mechi dhidi ya UD Songo na Kaizer Chiefs katika misimu miwili iliyopita ambazo zilifanya watupwe nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuhakikisha kambi yao hasa watakapokuwa ugenini inakuwa na ulinzi mkali wakilenga kuwaepusha wachezaji na maofisa wake wa benchi la ufundi na muingiliano na watu wengine wa kawaida ili kuepusha kuhujumiwa.

Mmoja wa viongozi wa Simba alilidokeza Mwanaspoti kuwa: “Tumejifunza mambo mengi sana katika msimu uliopita hasa tulipotolewa na Kaizer Chiefs kwenye hatua ya robo fainali na miongoni mwa hayo ni kuhakikisha kambi yetu haina muingiliano wa watu ambao unaweza kufanya hujuma kupenyezwa ndani ya timu.”

Kutokana na hilo, hoteli yetu tutakayofikia kule Botswana tutahakikisha inakuwa na ulinzi imara na hatutoruhusu watu ambao hatuwafahamu waisogelee lakini pia tutahakikisha huduma zote muhimu tunazisimamia wenyewe kama chakula na usafiri. Hata maji ya kunywa tutasafiri nayo na tutaenda na msafara mkubwa ili tuwe na watu wakutusaidia kwenye ulinzi,” alisema kiongozi huyo na kuongeza kwamba wanafanya mambo yao kitaalam sana na ndio maana wanakwenda kimyakimya. “Wale UD Songo hatukutegemea kama wangekuja kupata sare tasa hapa wakatutoa. Kaizer Chiefs nao tulicheza kwao tukiwa tumejiamini kupitiliza wakatufunga.”

Murtaza Mangungu ambaye Mwenyekiti wa Simba amelisisitizia Mwanaspoti kuwa malengo yao ni kufika mbali zaidi msimu huu na kila mechi kwao ina umuhimu na maandalizi yanaendelea kwa umakini mkubwa ingawa hakutaka kuingia kiundani.

MAJEMBE KIBAO SIMBA

Mzuka umerejea kambini Simba baada ya majembe yake yaliyokuwa majeruhi na wale wa timu ya taifa kurejea kambini huku wakimpa jeuri kocha Mkuu wa timu hiyo Didier Gomes.

Hapo awali mashabiki wa Msimbazi waliingiwa hofu juu ya kikosi chao kuelekea katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana baada ya nyota wake Shomari Kapombe, Sadio Kanoute, Pape Sakho, Kennedy Juma na Pascal Wawa kuumia lakini sasa kila mtu kapona.

Mwanaspoti jana liliweka kambi kwenye mazoezi ya Simba yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Beach Veterani na kushuhudia kila kitu ikiwemo mechi ya mazoezi ambayo Simba ilitoka sare ya bao 1-1 na Cambiasso Sports huku beki kisiki Hennoc Inonga Baka ‘Varane’ akitupia kwa kichwa bao la Simba dakika ya 19. Katika mechi hiyo Simba ambayo ilianza na kipa Beno Kakolanya, beki ya kulia alicheza U-20, kushoto Gadiel Michael huku kati wakisimama Erasto Nyoni na Varane.

Viungo walianza Jonas Mkude, Mzamiru Yassin na Ibrahim Ajibu huku mbele wakipangwa Benard Morrison, Jimmyson Mwanuke na Hassan Dilunga ambao walikiwasha kinoma.

Kipindi cha pili Simba ilifanya mabadiliko karibu ya kikosi kizima ili kuwapa nafasi wachezaji wengine ikiwemo wa U-20, na nyota Yusuph Mhilu, Abdulsamad Kassim, Ally Salim, Jeremiah Kisubi, Kapombe na Kanoute ambao waliingia na kukichafua kama kawaida.

Kapombe na Kanoute walirejea na kuwa fiti na kuonesha kiwango safi kwenye mechi hiyo huku kiungo Pape Sakho akiendelea mdogo mdogo na mazoezi ya kuweka sawa mwili.

Hata hivyo, kocha Gomes alisema: “Kanoute na Kapombe wako fiti na wanaendelea na programu za timu. Sakho anaendelea vizuri na nilipanga kumpa hata dakika 20 kwenye mechi ya leo (jana) dhidi ya Cambiasso kuona maendeleo yake licha ya kwamba ninauhakika Botswana atakuwepo.”

Sambamba na hayo pia Gomes amewazungumzia nyota wake waliokuwa katika timu zao za taifa, Aishi Manula, Kibu Denis, Mohamed Hussein, Kennedy Juma, John Bocco (Tanzania), Peter Banda, Duncan Nyoni (Malawi), Rally Bwalya (Zambia), Meddie Kagere (Rwanda), Taddeo Lwanga (Uganda) na Joash Onyango (Kenya) huku akijivunia walichokifanya.

“Nilitazama mechi ya Taifa Stars walionesha kiwango bora, Manula alikuwa kwenye kiwango bora.”