Simba mikononi mwa Kaizer Chiefs

Muktasari:

Simba imepangwa kucheza na Kaizer kwenye droo zilizochezeshwa leo jioni.

KLABU ya Simba imepangwa kucheza na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika zilizopangwa leo jioni.

Simba wataanza kutupa karata yao ya kwanza Mei 14 nchini Afrika Kusini kisha watarudiana Tanzania Mei 21-22 mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mabingwa hao watetezi wa Tanzania wameingia hatua ya robo fainali ya Mabingwa baada ya kumaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kundi A wakiwa na pointi 13.

Simba katika mechi sita za kundi hilo walishinda nne, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.

Mechi zingine ni Al Ahly dhidi ya Mamelod Sundowns, Mc Alger dhidi ya Wydad Club na Cr Belouizdad dhidi ya Esperance.