Simba kucheza na timu ya UEFA

KIKOSI cha Simba kabla ya kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara Januari 17, kikiwa huko Dubai kitacheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya timu kubwa kutokea maeneo tofauti.
Kocha wa Simba, Robertinho ametaka timu yake icheze michezo miwili dhidi ya timu kubwa na zenye wachezaji imara ili kupiga zile mbinu na mazoezi mbalimbali ambayo atakuwa anawapatia wachezaji wake.
Simba imethibitsha itacheza mechi ya kirafiki Januari 15 dhidi ya CSKA Moscow kutokea Urusi ambayo imekuwa ikicheza mashindano makubwa ya dunia kwa ngazi ya klabu kwa misimu mbalimbali.
CSKA Moscow imekuwa ikicheza UEFA Cup, UEFA Europa League, UEFA Super Cup na Uefa Champions league na mashindano mengine mbalimbali yale ya ndani na nje ya nchi yao.
Baada ya hapo Simba imepanga kujipima nguvu dhidi ya timu ya Al Dharfa ya Uarabuni saa 10:00 jioni Januari 13.
Kocha wa Simba, Oliviera Robertinho alisema anahitaji michezo hiyo ya kirafiki kwa ajili ya kuona mbinu na vitu mbalimbali ambavyo wanaelekeza wachezaji wake vinafanyiwa kazi.
Robertinho alisema miongoni mwa mbinu alizowapatia wachezaji wake na anataka kuziona kwenye michezo hiyo ya kirafiki ni kushambulia kwa kwa haraka, wanacheza kwa pamoja pindi wanapokuwa na mpira haswa eneo la kiungo.
Alisema kuna wakati anahitaji kuona maamuzi ya mchezaji binafsi yanatumika kutokana na mazingira yalivyo, kutawala mechi na kupata ushindi na kubadilisha mbinu kulingana na wapinzani walivyo.
"Bahati nzuri nimefika Simba nimekutana na wachezaji wazuri wenye vipaji vikubwa ambao naamini wanaweza kwenda kucheza na kukidhi kama falsafa zangu zilivyo ili kufikia malengo ya kutwaa mataji," alisema Robertinho na kuongeza;
"Bado mapema kuongea vitu vingi ila ngoja tuone kwanza ndani ya kipindi kifupi kuna mabadiliko yanatokea ndani ya timu haswa kwenye mechi na mazoezi na nimewaeleza wachezaji hilo wote kwa pamoja na mmojammoja kwamba nataka waonyeshe vipaji vyao,"
"Jambo lingine nimewaeleza wachezaji wangu wenyewe kwa wenyewe wanatakiwa kuwa na mahusiano mazuri, sitaki kuona wanatofautiana kwa namna yoyote ile jambo hilo litakuwepo kwetu benchi la ufundi na naamini nitaishi nao kama familia moja.
"Bahati nyingine nzuri tangu nimefika Simba nimekutana na ushirikiano mzuri kutoka kwa Juma Mgunda ambaye naye ana vitu vingi vya kiufundi na mbinu naamini nikiunganisha na vyangu timu inakwenda kufanya vizuri kwenye michezo mingi."