Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba icheki na mashine hizi!

Muktasari:

Mwanaspoti limeangazia mabeki hao wa kati ambao wanaweza kuchukua mikoba ya Erasto Nyoni na Pascal Wawa, baada ya Yusuph Mlipili na Kennedy Juma kushindwa kuonyesha umahiri wao. Hebu cheki listi hii:

KLABU ya Simba kupitia pendekezo la kocha wao, Sven Vandenbroeck eneo la beki wa kati nalo limeguswa kwa ajili ya kupatikana mchezaji ambaye atakwenda kuwa msaada kwa wakongwe Erasto Nyoni na Pascal Wawa.

Wakati Simba wanahaha kutafuta warithi au wasaidizi wa wachezaji hao, hapa hapa Bongo kuna mafundi kadhaa.

Mwanaspoti limeangazia mabeki hao wa kati ambao wanaweza kuchukua mikoba ya Erasto Nyoni na Pascal Wawa, baada ya Yusuph Mlipili na Kennedy Juma kushindwa kuonyesha umahiri wao. Hebu cheki listi hii:

BAKARY MWAMNYETO

Inaelezwa kwamba huu ndio utakuwa usajili wa kwanza wa Simba msimu huu, na tayari wameshabonga naye, ni ishu ndogo tu zimesalia. Ukitaja mabeki wa kati wenye uwezo mkubwa wa kupambana na kila aina ya washambuliaji huwezi kuacha kulitaja jina lake.

Mwamnyeto amekuwa mtulivu katika kupambana na washambuliaji. Hata Yanga wanamtamani na walishazungumza naye mara kadhaa, lakini dili halikumalizika kutokana na ishu za kimkataba. Lakini piga ua uwezekano wa yeye kutua Simba ni mkubwa safari hii.

ANDREW VICENT ‘DANTE’

Kwa uzoefu alionao bila shaka ni mtu sahihi pia kwenda kucheza na Pascal Wawa au Erasto Nyoni kama ambavyo alimpokea Nadir Haroub pale Yanga wakati anaamua kustaafu.

Dante anamaliza mkataba msimu huu na hajawa akipata nafasi kwenye kikosi cha kwanza na uwepo wa ushindani wa namba ni rahisi kwake kuweza kuchomoka kutafuta maisha sehemu nyingine. Aliyumba kutokana na misimamo yake Yanga akidai pia masilahi yake.

Simba wanaweza wakaanza kupiga chapuo kwa beki huyu kwani uwezo wake unajulikana pindi anapokuwa uwanjani na umri wake pia wanaweza wakawa naye kwa muda mrefu na inawezekana ikawa ni rahisi kuchomoka kwani mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu.

DAVID MWANTIKA

Ni beki mwili jumba na amedumu ndani ya Azam kwa muda mrefu mpaka msimu huu benchi la ufundi lilipoweka wazi kwamba hayupo kwenye mipango yao. Wamempeleka kwa mkopo Lipuli, lakini hakwenda anaendelea kujifua kivyake uswazi na mkwanja wake unaingia kama kawaida kutoka Azam.

Mwantika ni beki kisiki na amekuwa bora katika wakati wote ule tangu yupo Prisons mpaka anasajiliwa Azam Fc.

Ni kisiki kwelikweli na msimu huu mkataba wake unamalizika, inaelezwa kwamba hayupo kwenye furaha katika kikosi cha Azam FC kutokana na kutolewa kwa mkopo, hivyo inaweza ikawa njia nzuri ya kutoka kwenda Simba.

IDD MOBBY

Ni beki mtulivu na aliwahi kujumuishwa katika kikosi cha timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa stars’ hivi karibuni, lakini baadaye akaondolewa na kubaki Bakari Mwamnyeto.

Mobby, umri wake ni kijana na amekuwa bora kwa kipindi chote tangu akiwa anaichezea Mwadui FC iliyokuwa inanolewa na Ally Bizimungu mpaka hivi sasa akiwa na kikosi cha Polisi Tanzania.

Simba mara kwa mara walikuwa wanatajwa kuwinda saini yake wakati akiwa na Mwadui FC. Hivi sasa inawezekana ameshakomaa kutokana na Ligi Kuu kuwa tayari ameshaifahamu vya kutosha.

MOHAMED KASSIM

Akiwa katika kikosi cha Polisi Tanzania msimu huu ameonyesha ubora wa hali ya juu, na katika kikosi hicho akicheza sambamba na Idd Mobby.

Umakini wake kwenye uwanja na umri wake ni vitu viwili tofauti. Kama Simba wamekuwa wakimfuatilia au watamfuatilia kwenye mechi zilizobaki wanaweza kuona kipaji chake na kukichukua kwa ajili ya usaidizi kwa Wawa na Erasto.

Polisi wanapambana hivi sasa kuona namna gani ambavyo wanaweza wakambakiza katika kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao kwani amekuwa na msaada mkubwa katika safu yao ya ulinzi.

ABDALLAH KHERI ‘SEBO’

Ukimuona huyu jamaa ndani ya timu ya Taifa ya Zamzibar ‘Zanzibar Heroes’ unaweza ukashangaa kinachomtokea Azam FC kwa sasa.

Staili ya uchezaji ya Kocha Aristica Cioaba wa Azam FC bado haijamuelewa, ndio maana hajaingia kwenye kikosi cha kwanza mara kwa mara. Amempotezea na kuwatumia Yakub Mohamed na Aggrey Morris na wakati mwingine Oscar Masai.

Lakini jamaa ni bonge la beki na kwa timu ngumu kama Simba anaweza kupambana na kuonyesha kitu.

Ni beki mtulivu na ana uwezo mkubwa wa kupambana, kukosa kwake nafasi katika kikosi cha kwanza kunaweza kumpa nafasi ya kutua Simba hata kwa mkopo na akafanya mambo.

Kheri pia ni beki wa timu ya Taifa Zanzibar na akiwa ndani ya jezi za timu hiyo ubora wake umekuwa maradufu.