Simba: Hii gemu imeisha

MASHABIKI wa Simba wanahesabu saa tu kabla ya kushuhudia chama lao likishuka uwanjani kuvaana na RS Berkane ya Morocco katika mechi za Kombe la Shirikisho Afrika, huku kocha Pablo Franco akimaliza kazi mapema.
Pablo alimaliza kazi hiyo mazoezini kwa kuwapigisha tizi la maana lenye mbinu za kuhakikisha wanalipa kisasi dhidi ya Wamorocco, huku mastaa wa timu hiyo wakiapa kwamba Berkane hawatoki salama Kwa Mkapa.
Kwenye mazoezi, Pablo alionekana kuvifanyia kazi vitu vitatu, kufunga mabao mengi kulingana na nafasi watakazotengeneza, kukaba kuanzia juu na wakipata mpira hakuna kupoteza wanatakiwa kupasiana haraka na kutengeneza shambulizi ya hatari.
Katika zoezi la kufunga mabao Chris Mugalu alionekana kufanya vizuri akiwatungua makipa, Aishi Manula na Benno Kakolanya wakati Meddie Kagere alionekana kupoteza nafasi na kushindwa kupiga mashuti mengi yaliyolenga lango.
Kwenye zoezi la kukaba kuanzia mbele, Pablo alitaka kumuona Peter Banda, Pape Sakho, Bernard Morrison na Kagere wanaanza kuwakaba mabeki wa RS Berkane ili wawazuie kucheza kuanzia nyuma na kupiga mipira mirefu. Wachezaji wa Simba baada ya kupata mpira walitakiwa kushambulia kwa haraka na kasi huku Banda, Sakho na Morrison wakitumika zaidi kwenye kutengeneza mashambulizi ya hatari na ikiwezekana kufunga wenyewe.
Nahodha wa Simba, John Bocco hatakuwa sehemu ya kikosi dhidi ya RS Berkane na hakuwa sehemu ya mazoezi kwani amepewa mapumziko kutokana na majeraha ya misuli ya nyuma nyama za paja aliyoyapata katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji na kushindwa kuendelea na mchezo na kutolewa kipindi cha kwanza.
Kulingana na mazoezi hayo taarifa njema katika kikosi cha kwanza Simba kiungo mkabaji, Taddeo Lwanga anaweza kupewa nafasi ya kuanza kama hakutakuwa na mabadiliko.
Kikosi cha Simba kitakuwa tofauti kabisa na kile lichoaanza katika mechi ya kwanza ugenini Morocco kilichokuwa na Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Joash Onyango, Henock Inonga, Kennedy Juma, Pape Sakho, Erasto Nyoni, John Bocco, Sadio Kanoute na Peter Banda.
Kikosi hicho cha mechi ya kwanza kilikuwa na mlengo wa kucheza kwa kujilinda zaidi ndio maana Pablo alianza na mabeki wa kati watatu, wakati kesho amefanya mabadiliko na ataanzisha cha kushambulia zaidi.
Kikosi kinachoweza kuanza kesho kina, Manula, Kapombe, Hussein, Onyango, Inonga, Lwanga, Sakho, Kanoute, Kagere, Morrison na Banda.
Kocha Pablo alisema: “Kulingana na mahitaji makubwa ya ushindi katika mchezo huu wa nyumbani ndio maana tumefanya mabadiliko ya kiufundi.”
WASIKIE MASTAA
Manula alisema: “Tunatambua ni mchezo mgumu, tunajivunia mashabiki wetu tunawaomba waje kwa wingi.”
Kapombe alisema: “Hakuna timu nyepesi tunachotakiwa wachezaji ni kupambana kushinda na kukaribia malengo.”
Naye Nyoni aliwaita mashabiki ili wawe sehemu ya mchezo.
Imeandikwa na Thobias Sebastian, Clezencia Tryphone, Oliver Albert, Charles Abel na Khatimu Naheka