SIMBA DAY: Mechi zilizopita tamashani

LICHA ya usajili kushamiri katika kila timu nchini lakini tukio la ‘Simba Day’ linaleta hamasa kwa mashabiki wa Simba kujiuliza kile kitakachotokea siku hiyo.

Tamasha hilo hufanyika Agosti 8 ya kila mwaka tangu lilipoasisiwa na viongozi wa zamani wa Simba, na Mwina Kaduguda.

Mwaka 2014 lilifanyika Agosti 9 kutokana na matatizo yaliyojitokeza. Hapa Mwanaspoti linakuletea orodha ya michezo iliyochezwa katika tamasha hilo tangu kuanzishwa kwake 2009.


Simba 1-0 SC Villa (2009)

Hii ndiyo mechi ya kwanza kuchezwa katika Simba Day na Simba kushinda bao 1-0 dhidi ya SC Villa ya Uganda.

Bao la Simba lilifungwa na kiungo, Hilary Echessa dakika ya nane ya akiwa amesajiliwa kwa mara ya kwanza kutoka timu hiyo aliyoifunga (SC Villa) katika Uwanja wa taifa (sasa Uhuru).

Katika msimu huo wa Ligi Kuu, Simba ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara bila kufungwa ikiwa chini ya Mzambia, Patrick Phiri ukiwa ni msimu wa kwanza pia kwa wachezaji Emmanuel Okwi na Joseph Owino.


Simba 0-0 Express (2010)

Tamasha la pili lilifanyika na Simba ilitoka suluhu na wageni kutoka Uganda, Express.

Katika msimu huu Simba bado ilikuwa ikinolewa na Mzambia, Phiri na baadhi ya nyota wake walikuwa, George Owino, Ally Mustafa (Bathez), Emmanuel Okwi.


Simba 0-1 Victors (2011)

Tamasha hili lilifanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha na Simba ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Victors ya Uganda. Bao lilifungwa kwa penalti na Patrick Sembuya. Simba ilikuwa chini ya Kocha Mserbia, Milovan Cirkovic.


Simba 1-3 Nairobi City (2012)

Hii ilikuwa ni mara ya pili Simba ikiwa chini ya Cirkovic kufungwa tena katika Simba Day. Ilifungwa mabao 3-1 na Nairobi City Stars ya Kenya. Mabao yalifungwa na Duncan Owiti, Bruno Okullu na Boniphace Onyango (79) huku la kufutia machozi kwa Simba likifungwa na Felix Sunzu.


Simba 4-1 SC Villa (2013)

Awamu hii Simba ilionyesha mabavu yake na kuisambaratisha SC Villa ya Uganda 4-1. Mchezo ulipigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam chini ya Kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni.

SC Villa ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tisa kupitia kwa Mganda Robert. Mabao ya Simba yalfungwa na Jonas Mkude, William Lucian na Betram Mombeki aliyefunga mawili (70) na (72).


Simba 0-3 Zesco (2014)

Hiki ni kipigo cha tatu kwa Simba tangu tamasha hili lilipoanzishwa. Mabao ya Zesco ya Zambia, yalifungwa na Jackson Mwanza, Clatos Chane na Mayban Mwamba.


Simba 1-0 SC Villa (2015)

Hii ni mechi ya saba kwenye tamasha hili na ya tatu kwa timu hizi kukutana. Simba ilihinda bao 1-0 lililofungwa na Awadh Juma.


Simba 4-0 AFC Leopards (2016)

Katika mchezo huu Simba iliialika AFC Leopard kutoka Kenya na kushinda mabao 4-0 yaliyofungwa na Ibrahim Ajibu aliyefunga mawili, Laudit Mavugo na Shiza Kichuya.


Simba 1-0 Rayon Sports (2017)

Huu ulikuwa misimu tisa wa Simba Day. Timu hiyo ilishinda bao 1-0 dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda. Bao hilo lilifungwa na kiungo Mohamed Ibrahim akipokea pasi ya mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi.


Simba 1-1 Kotoko (2018)

Hii ilikuwa mechi ya pili kwa Simba kucheza na timu kutoka nje ya Afrika Mashariki baada ya Zesco ya Zambia (2014). Simba ilishindwa kutamba dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana baada ya kufungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Benjamin Mkapa).


Simba 3-1 Power Dynamos (2019)

Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Power Dynamos kutoka Zambia huku Meddie Kagere akifunga mabao yote matatu (hat-trick).


Simba 6-0 Vital’O (2020)

Huu ni ushindi mkubwa kwa Simba dhidi ya Vital’O ya Burundi. Mabao yake yalifungwa na Bernard Morrison, John Bocco, Clatous Chama, Ibrahim Ajibu, Chris Mugalu na Charles Ilamfya.


Simba 0-1 TP Mazembe (2021)

Katika tamasha hili Simba ilifungwa bao 1-0 na TP Mazembe kutoka Lubumbashi Congo kwa bao la Tik-taka la Jean Baleke.


MAONI YA WADAU

Akizungumzia tamasha hilo aliyekuwa mchezaji wa kikosi hicho, Mussa Hassan Mgosi amesema anatamani mashabiki wa timu hiyo waondokane na mawazo ya msimu uliopita ili waweze kuwasapoti wachezaji wao kwa ajili ya msimu mpya wa 2022/23.

“Msimu uliopita timu ilimaliza nafasi ya pili, hivyo wanatakiwa waungane tena kuisapoti, uongozi, wachezaji pamoja na kuiombea ili iweze kutwaaubingwa.”

Mchezaji na kocha wa zamani wa kikosi hicho, Abdallah ‘King’ Kibadeni amesema; “Usajili wa msimu huu umekuwa wa siri, kuna wachezaji walitajwa kuachwa na wengine kuongezwa ila uhakika zaidi utapatikana siku hiyo,” alisema Kibadeni na kuongeza;

“Mwaka huu Simba wasiwasahau wachezaji wa zamani ambao wametoa jasho lao kuhakikisha inakuwa Simba. Wapewe heshima yao katika tamasha hilo, wapo wazee wengi kama kina Hassan Dalali, mimi angalau wakumbukwe na ikiwezekana tuwe wageni kuliko kuwaleta wengine kutoka nje.”