Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba Chupuchupu, URA yaua

Muktasari:

Timu zote zilishambuliana kwa zamu, huku Jamhuri ikiifunika kabisa Simba kwa soka murua, ingawa hadi zikienda mapumziko matokeo yalikuwa bao 1-1.

MABINGWA watetezi wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, Simba imeanza vibaya baada ya usiku wa jana Jumatatu kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na timu ya Jamhuri Pemba katika pambano la Kundi A la michuano hiyo uliochezwa Uwanja wa Amaan.

Simba ambayo ilichezesha asilimia kubwa ya wachezaji walizoeshwa benchi, ilianza kuandika bao la mapema dakika ya 13 kupitia Awadh Juma ‘Maniche’ kabla ya Jamhuri kusawazisha dakika tano kwa mkwaju mtamu uliotumbukizwa na Mwalimu Khalfan.

Timu zote zilishambuliana kwa zamu, huku Jamhuri ikiifunika kabisa Simba kwa soka murua, ingawa hadi zikienda mapumziko matokeo yalikuwa bao 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa Jamhuri kuipeleka puta Simba na kuandikisha bao la pili dakika ya 54 kupitia kwa Ammy Bangaseka aliyemalizia krosi pasi ya Mwalimu.

Hata hivyo mabadiliko ya wachezaji yaliyofanywa na Kocha Dylan Kerr ya kuwatoa Issa Said, Joseph Kimwaga na Mussa Mgosi na kuwaingiza Emiry Nimuboma,  Mwinyi Kazimoto na Danny Lyanga iliisaidia Simba kurejesha uhai na kuikimbiza Jamhuri. Jitihada ya mashambulizi ya Msimbazi yalizaa matunda baada ya Awadh Juma kwa mara nyingine kuifungia Simba bao la kusawazisha katika dakika ya 77.

Kuingia kwa bao hilo kulifanya mchezo kuchangamka zaidi kila timu ikisaka bao la ushindi na kuwepo kosa kosa nyingi hasa langoni mwa Jamhuri, lakini umakini mdogo wa mastraika wa Simba uliikosesha timu hiyo bao na hivyo dakika 90 kuisha kwa sare.

Katika mechi ya mapema jana Jumatatu jioni, URA ya Uganda ilipata ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya JKU ya Unguja katika pambano lililokuwa tamu.

URA ilipata mabao yake kupitia kwa Oscar Aggaba aliyefunga dakika ya 12 na Villa Oromuchan aliyefunga mawili katika dakika ya 21 na 77. Bao pekee la kufutia machozi la JKU lilitimiwa kimiani na Mohammed Abdallah dakika ya 18.

Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo Jumanne kwa michezo miwili ya Kundi  B, jioni Mtibwa itakwaruzana na Mafunzo na usiku Azam na Yanga zitamaliza ubishi.