Simba: Chekeni tu, sisi bado tupo Kimataifa

Monday October 25 2021
simba pic
By Charity James

SIMBA imepoteza mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya siku 3,171 na kusababisha mashabiki wachache wa Yanga waliokuwa uwanjani kushangilia sana, lakini wapinzani wao kuwajibua wakiwaambia; ‘Nyie chekeni, lakini sisi bado tupo kimataifa’.

Wekundu hao walipasuka mabao 3-1 na kung’olewa kwenye Ligi ya Mabingwa, lakini wakaangukia katika play-off ya Kombe la Shirikisho Afrika ili kusaka nafasi ya kucheza makundi kuyasaka mamilioni ya fedha za wadhamini wa michuano hiyo ya pili kwa ukubwa Afrika kwa ngazi ya klabu.

Ikishuka uwanjani ikiwa na hazina ya mabao 2-0 iliyopata kwenye mchezo wa kwanza, Simba ilionyesha kujiamini kupita kiasi, huku kukiwa hakna mabadiliko yoyote katika kikosi kilichocheza Gaborone, Botswana wiki iliyopita.

Kuonyesha nyota wa Simba waliamini walishamaliza kazi Botswana, winga wao Mghana dakika za mapema kabisa alianza mbwembwe zake za kuupanda mpira na kuwafanya ashangiliwe na mashabiki, lakini baada ya dakika 90 mashabiki hao hao wa Simba walikuwa wanyonge baada ya timu kulala.

Simba ilikuwa haijawahi kupoteza mechi yoyote ya kimataifa kwenye uwanja wa nyumbani tangu ilipofungwa bao 1-0 na Recreativo do Libolo ya Angola katika mechi iliyopigwa Februari 17, 2013.

Simba ilianza kupata bao la kuongoza dakika ya 41 kupitia kwa kiungo wake fundi, Rally Bwalya, bao lililodumu hadi mapumziko, lakini kipindi cha pili kilipoanza wageni walioingia na tofauti na wachezaji wawili tofauti na kikosi kilichocheza nyumbani kwao, ilicharuka, hasa baada ya kocha wao kufanya mabadiliko.

Advertisement

Kocha huyo aliwatoa Thabang Vicent na Themba Dhladhla na kuwaingiza Tshephang Boithatelo na Rudath Wendell waliobadilisha kabisa kasi ya mchezo kwani dakika moja baada ya kuingia kwa wachezaji hao Galaxy ilipata bao la kusawazisha. Bao hilo liliwekwa kimiani na Wendel kabla ya kuongeza jingine la pili dakika 59 akitumia makosa ya mabeki wa Simba walioshindwa kuokoa mpira wa kurushwa na kufunga bao lililoshangiliwa na mashabiki wachache wa Yanga.

Licha ya Simba kucharuka kutaka kurudisha bao hilo hasa baada ya kocha Hitimama Thiery aliyekuwa benchi kutokana na Didier Gomes alikuwa jukwaa kufanya mabadiliko ya kuwatoa kina Hassan Dilunga na kumuingiza Peter Banda na baadaye kumtoa Morrison kumuingiza Duncan Nyoni na baadaya John Bocco ili kumpisha Meddie Kagere, Taddeo Lwanga kumpisha Ersto Nyoni.

Hata hivyo dakika ya 86 wakati mashabiki wakiamini Simba inaenda makundi, Gape Mohutsiwa alifunga bao la kichwa na kuiny’ongesha Simba kwani ilifanya matokeo ya jumla kuwa 3-3 na Simba kutolewa kwa faida ya bao la ugenini lililowanufaisha Galaxy.

Matokeo hayo yamejirudia na misimu miwili iliyopita, Simba ikitoka kucheza robo fainali ilitolewa raundi ya awali na UD Songo ya Msumbiji kwa bao la faida ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya 1-1 ikiwa ni siku chache ilipolazimisha suluhu Maputo.

Hiki ni kipigo cha kwanza kwa Simba kati ya mechi 14 ilizocheza nyumbani tangu ilipofungwa 2013, kwani ilishinda michezo 10 na kupata sare tatu.


MAMILIONI YA CAF

Kipigo kimeifanya Simba ikose mamilioni ya ya CAF kwani kama ingetinga makundi ingejihakikisha kubeba Dola 550,000 (sawa na Sh 1.2 bilioni) na sasa italazimika kupambana kwenye play off ili kuitafuta tijketi ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Hata hivyo Simba itabidi ifanye kazi kwa bidii kwani kwenye timu zilizofuzu 16 Bora (play-off) ya Shirikisho sio za kitoto, kwani hadi jana kulikuwa na timu za CS Sfaxien ya Tunisia, JS Saoura ya Algeria, Pyramids na Al Masry ya Misri, Enyimba ya Nigeria, Murumo Gallants ya Afrika Kusini, Coton Sport ya Cameroon, Binga FC ya Mali na Gor Mahia ya Kenya.

Pia kulikuwa na uwezekano wa timu za US Ben Guernade ya Tunisia au RS Berkane ya Morocco kutinga kutegemeana na matokeo ya usiku wa jana ilivyo kwa FAR Rabat ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria zilizokuwa zikirudiana.

Timu zinazotoka Ligi ya Mabingwa hukutana na zile zilizofuzu 16 Bora ya Kombe la Shirikisho kuwania nafasi ya kuingia makundi ambapo msimu uliopita Nanungo ilifuzu na kuandika rekodi yao, ikicheza mechi zote sita bila kufunga bao lolote wala kuambulia pointi moja.


MO AVUNJA UKIMYA

Mara baada ya pambano hilo mashabiki wa Simba wakishindwa kuamini na kutumia muda mrefu kutoka uwanjani, huku baadi yao wakimtaja Clatopus Chama na Luis Miquissone kwamba mapengo yao ya kuuzwa Misri na Morocco bado hayajazibika kwani wanaamini Galaxy haikuwa timu ya kuwang’oa Ligi ya Mabingwa ikiwa nyumbani, huku Bilionea wa klabu hiyo, MOhammed ‘Mo’ Dewji akiandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa twitter kwamba ‘Amefadhaishwa sana’, kuonyesha matokeo hayo yamemchanganya tofauti na tumaini lake, ikiwa ni muda mchache baada ya mchezo huo.

Advertisement