Simba, Azam zajitosa Kombe la Muungano, Yanga yachomoa!

Muktasari:

  • Simba na Azam zilizopo katika Ligi Kuu Bara ndizo timu pekee za Tanzania Bara zilizothibitisha kushiriki katika michuano hiyo itakayoshirikisha pia timu za visiwani Unguja na Pemba.

KLABU za Simba na Azam FC zimethibitisha kushiriki michuano ya Kombe la Muungano inayoenda sambamba na Miaka 60 ya Sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitakazoadhimishwa Aprili 26, huku Yanga ikichomoa.

Simba na Azam zilizopo katika Ligi Kuu Bara ndizo timu pekee za Tanzania Bara zilizothibitisha kushiriki katika michuano hiyo itakayoshirikisha pia timu za visiwani Unguja na Pemba.

Simba iliyopo nafasi ya tatu na Azam ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara zimethibitisha kushiriki michuano hiyo itakayoanza  Aprili 23.

Akizungumza na Mwanaspoti, Rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar(ZFF), Suleiman Mahmoud amesema, walikuwa kimya kwa muda kusubiri taarifa ya Simba kama watakuwepo au la, huku ya Azam ikithibitisha mapema ushiriki wao.

Rais hiyo ZFF amesema, Yanga walitoa taarifa  mapema kuwa hawataweza kushiriki kutokana na ratiba  iliyonayo msimu  huu.

“Nia ya michuano hii ni kuinua uhusiano kati ya Bara na Zanzibar kwa upande wa soka, lakini  kuimarisha timu zetu za huku na biashara kwa ujumla  kwani timu kubwa zinapocheza huwa kuna watazamaji na watalii wengi wanaokuja Zanzibar, amesema Suleiman na kuongeza;

"Bila kusahau kuongeza tuzo na uimara wa wachezaji, kwani wanapocheza michezo tofauti na yenye ushindani wa aina hii basi ni mazoezi tosha ya kujiboresha zaidi.

"Ni fursa kwa vipaji vilivyoko Zanzibar, kupata nafasi ya kuonekana na watu wengi hivyo ni rahisi kwao kupata ajira na kujulikana.” amesema.

Ratiba ya michuano hiyo inatarajiwa kutolewa baada ya kumalizika kwa mtanange wa Yanga na Simba utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii, Aprili 20 Kwa Mkapa.

Mbali na Simba na Azam timu nyingine shiriki kwa mujibu wa Suleiman ni mabingwa Zanzibar KMKM na KVZ.

Michuano hiyo itachezwa kwenye Uwanja mpya wa New Amaan Complex na fainali itachezwa Aprili 27  siku moja baada ya sherehe za maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano.
Tanganyika na Zanzibar ziliungana Aprili 26, 1964 na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa kwa sasa na Rais Samia Suluhu Hassan.