Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, Azam FC rekodi zinaongea

MECHI ZILIVYO
2008-2009
Okt 4, 2008    Simba     0-2         Azam
Mar 30, 2009    Azam     0-3         Simba
2009-2010
Okt 24, 2009    Simba     1-0         Azam
Mar 14, 2010    Azam     0-2         Simba
2010-2011
Sept 11, 2010    Azam     1-2         Simba (Tanga)
Jan 23, 2011    Simba     2-3         Azam
2011-2012
Sept 11, 2011     Azam     0-0         Simba
Feb 11, 2012     Simba     2-0        Azam
2012-2013
Okt 27, 2012     Simba      3-1         Azam
Apr 14, 2013    Azam     2-2         Simba
2013-2014
Okt 28, 2013     Simba     1-2         Azam
Mar 30, 2014     Azam     2-1         Simba
2014-2015
Jan 25, 2015     Azam     1-1         Simba
Mei 21, 2015     Simba     2-1         Azam
2015-2016
Dec 25, 2015     Azam     2-2         Simba
Mei 11, 2016-    Simba     0-0         Azam
Msimamo wa jumla baina yao
                 P      W      D      L      F       A      Pts
Simba      16      7      5       4      24     17     26
Azam       16      4      5       7      17      24     17

Muktasari:

  • Tayari mashabiki wameshakaa mkao wa kula kupata burudani na kutaka kushuhudia wanaume 22 wa timu hizo wakitoana jasho kwenye mchezo huo wa kwanza msimu huu.

MASHABIKI wa soka walitaka kuzinguliwa wakati wakijiandaa kupata burudani wikiendi hii kiasi cha kufikia kusonya kwa hasira huko walipokuwa. Unajua kwa nini?  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitaka kuwakatishia uhondo kwa kutaka kuahirisha pambano kali la Simba na Azam lililopangwa kufanyika Jumamosi hii.

TFF ilitangaza kusitisha pambano hilo mpaka wiki ijayo ya Septemba 24 kisa, kupisha mchezo wa kimataifa ya timu ya taifa ya Vijana U17 ‘Serengeti Boys’ dhidi ya Congo, lakini baada ya viongozi wa timu zote kugomea ubabaishaji huo TFF imesarenda. Kinyonge imeruhusu pambano hilo sasa lipigwe kama kawaida, ila kutoka Uwanja wa Taifa mpaka Shamba la Bibi, Uwanja wa Uhuru, kitu kilichowafanya mashabiki huko mitaani kushangilia kwa kuamini kuwa mechi hiyo ndio fainali ya kubashiri bingwa.

Tayari mashabiki wameshakaa mkao wa kula kupata burudani na kutaka kushuhudia wanaume 22 wa timu hizo wakitoana jasho kwenye mchezo huo wa kwanza msimu huu. Hakuna ubishi pambano baina ya Azam na Simba lina mvuto na msisimko wake kiasi kwamba huziweka juu juu roho za mashabiki kutokana na utamu wake na ushindani baina ya timu hizo tangu Azam ipande Ligi Kuu mwaka 2008.

Mwanaspoti linakuletea rekodi mbalimbali za mipambano 16 ya awali ya ligi baina ya timu hizo tangu msimu wa 2008-2009 na ubashiri wa mchezo huo wa 17 kulingana na uimara wa vikosi vya timu hizo zilizopo kileleni kwa sasa katika Ligi Kuu Bara.

KINARA

Katika michezo 16 iliyochezwa baina ya timu hizo, Simba inaongoza kwa kushinda mara nyingi ikilinganishwa na wapinzani wao, kwani Wekundu wa Msimbazi wameshinda mara saba, huku Azam ikishinda mara nne tu.

Katika mechi hizo saba, Simba imeshinda mara tatu ugenini sawa na wapinzani wao, huku michezo yake mingine iliyosalia ikishinda nyumbani, wakati wapinzani wao wameshinda mechi moja tu ikiwa nyumbani.

Azam ndiyo klabu iliyolazimishwa sare nyingi nyumbani kati ya michezo mitano iliyoshindwa kutoa mshindi baina yake na Simba, kwani imefanya hivyo mara nne dhidi ya moja ya Simba ikiruhusu kugawana pointi kwao.

Pambano moja tu kati ya vidume hao limechezwa nje ya Jiji la Dar es Salaam, nalo ni lile lililochezwa Septemba 11, 2010 uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga, uliotumiwa kama Uwanja wa nyumbani wa Azam na kulala 2-1.

Pia kama hujui ni kwamba ni pambano moja tu ambalo liliwahi kuchezwa kwa siku mbili mfululizo. Mchezo huo ni ule wa uliopigwa Machi 29, 2009 na kulazwa baada ya kipindi cha kwanza kutokana na mvua kubwa ambapo Simba iliongoza kwa bao 1-0.  Bao hilo liliwekwa kimiani na Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na mchezo kurudiwa Machi 30 na  Simba ikaikandamiza Azam kwa mabao 3-0 na kulipa kisasi cha kipigo cha mchezo wao wa awali walipolala mabao 2-0.

MABAO

Katika mechi hizo 16 wanaume hao wamezalisha jumla ya mabao 41, huku Simba ikiongoza kwa kufumania nyavu za wapinzani wao, ikifanya hivyo mara 24 dhidi ya 17 iliyofunga Azam.

Katika mabao hayo 41 yaliyofungwa katika mechi za timu hizo, mchezaji mmoja tu ndiye aliyewahi kujifunga naye ni beki Aggrey Morris aliyejifunga katika mechi iliyochezwa Oktoba 24, 2009 ambapo Azam ililala ugenini kwa bao 1-0.

Aidha pambano lililochezwa Januari 23, 2011 ndilo lililozalisha mabao mengi katika mchezo mmoja, yakifungwa jumla ya mabao matano katika matokeo ya 3-2 Azam ikishinda ugenini.

Michezo miwili tu, wa Septemba 11, 2011 na mchezo wa marudiano wa msimu uliopita uliopigwa Mei 11, 2016 ndio ambayo haukuzalisha mabao baada ya timu hizo kushindwa kufungana. Lakini sare yenye mabao mengi baina ya timu hizo ni zile zenye matokeo ya 2-2 zilizopatikana kwenye pambano la kwanza la msimu uliopita lililochezwa Desemba 12, 2015 na mchezo wa Aprili 14, 2013.

WAFUNGAJI

Katika mabao 41 yaliyopatikana katika mechi 16 zilizopita, straika John Bocco ‘Adebayor’ ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi. Bocco amefunga mara sita katika mechi baina ya timu yake dhidi ya Simba, akifuatiwa na Kipre Tchetche ambaye kwa sasa hayupo Azam mwenye mabao manne. Bocco alifikisha idadi hiyo alipofunga mabao mawili katika mechi ya kwanza ya msimu uliopita, huku Ibrahim Ajib akiifungia Simba katika mechi iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.

Katika pambano hilo la msimu uliopita Bocco na Ibrahim Ajib kila mmoja alifunga mabao mawili ya timu hizo, kitu ambacho hakikuwahi kutokea kabla kwa wachezaji wawili tu kufunga mabao manne ya mchezo mmoja.

Winga wa sasa wa Simba, Jamal Mnyate ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao katika mechi baina ya timu hizo. Mnyate alifunga bao katika pambano la kwanza kwa timu hizo msimu wa 2008 mchezo uliochezwa Oktoba 4, 2008 ambapo Simba ilicharazwa nyumbani mabao 2-0. Mnyate alifunga katika dakika ya 42 kabla ya Shekhan Rashid kuongeza la pili kwa penalti dakika ya 90+5.

Mkenya Mike Barasa ndiye mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili katika pambano moja baina ya timu hizo akifanya hivyo katika mechi ya Machi 14, 2010 wakati Simba ikishinda ugenini mabao 2-0.

UBASHIRI

Kwa namna vikosi hivyo vilivyojengeka msimu huu, pambano hilo la Jumamosi ni gumu kutabirika, lakini timu yoyote itakayofanya makosa uwanjani ni lazima itaadhibiwa, japo Azam inapewa nafasi kubwa ya kupunguza vipigo dhidi ya Simba.

Simba itakuwa na kazi ya kumzuia Bocco na Ya Thomas walioanza msimu kwa makeke, huku Azam ikiwa na kazi kubwa ya kuwachunga Laudit Mavugo, Ajib na Shiza Kichuya walio wasumbufu na wanashirikiana vyema uwanjani kuibeba Simba.