Yanga yaizamisha Mashujaa Kigoma, ikiusogelea ubingwa Ligi Kuu
Muktasari:
- Katika mechi hiyo iliyokuwa ya vuta nikuvute kutokana na ushindani wa timu zote mbili, Mudathir alifunga bao hilo nje ya eneo la 18, baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa kikosi cha maafande, Lameck Kanyonga na kuingia nyavuni.
MABAO mawili likiwamo kali la dakika ya 27, lililofungwa na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mudathir Yahya na la nahodha Bakari Mwamnyeto yalitosha kuipa timu hiyo pointi tatu muhimu katika mechi kali ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa FC, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Katika mechi hiyo iliyokuwa ya vuta nikuvute kutokana na ushindani wa timu zote mbili, Mudathir alifunga bao hilo nje ya eneo la 18, baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa kikosi cha maafande, Lameck Kanyonga na kuingia nyavuni.
Ubora wa bao hilo la Mudathir aliyefikisha mabao tisa ya Ligi Kuu msimu huu wa 2025-2026, ulitokana na mpira kuguswa na nyota watatu akipiga kipa, Djigui Diarra na kupigwa kichwa na Prince Dube na kumkuta nyota huyo aliyepiga shuti kali.
Mabingwa hao watetezi wa michuano hiyo, ilipata bao la pili dakika ya 90 lililotokana na mpira wa piga ni kupige langoni mwa Mashujaa baada ya shuti la Maxi Nzengeli kuokolewa na kipa Lameck Kanyonga, kabla ya kumrudia na kupiga tena na katika harakati za kuokoa, Mwamnyeto akausukumiza golini.
Mechi ya raundi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Yanga ilishinda mabao 6-0, Januari 19, 2026, yaliyofungwa na Mohamed Damaro, Duke Abuya, Prince Dube, Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya na Laurindo Dilson Maria ‘Depu’.
Kwa maana hiyo, Yanga ilikutana na Mashujaa ikiwa na kumbukumbu nzuri pia, huku kwa upande wa kikosi hicho cha maafande kikikabiliwa na mwenendo usioridhisha, baada ya kucheza mechi tano mfululizo za Ligi Kuu Bara hadi sasa bila ya ushindi.
Katika mechi hizo tano ilizocheza Mashujaa FC bila ya kushinda, imepoteza tatu na kutoka sare mbili, huku mara ya mwisho kwa kikosi hicho cha maafande kushinda ilikuwa ushindi wa bao 1-0, dhidi ya TRA United ikicheza nyumbani, Mei 4, 2026.
Mbali na hilo, Mashujaa imeendeleza rekodi mbovu, kwani timu hiyo ya maafande tangu ipande Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024, haijawahi kuifunga Yanga kwani zimekutana mara sita na kuchapwa zote, ikiruhusu mabao 19 na kufunga matatu.
Katika mechi 26 za msimu huu wa 2025-2026, Yanga imeshinda 19, sare sita na kupoteza moja ikiongoza msimamo na pointi 63, huku kwa upande wa Mashujaa FC ikiwa nafasi ya 11 na pointi 27, baada ya kushinda tano, sare 12 na kupoteza tisa.
CITY YALIPA KISASI
Katika mechi ya mapema iliyopigwa saa 8:00 mchana Uwanja wa Sokoine, jijini, Mbeya, wenyeji Mbeya City iliibuka na ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Mtibwa Sugar lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na nyota, Adilly Buha dakika ya 36.
Timu hizo zilikutana zikiwa na mwenendo usioridhisha na Mbeya City ilicheza mechi nne mfululizo za Ligi Kuu bila ya ushindi, tangu mara ya mwisho ilipoifunga maafande wa Tanzania Prisons mabao 2-1, Mei 4, 2026.
Kwa upande wa Mtibwa Sugar imefikisha mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu bila ya ushindi na kati yake imepoteza mbili na kutoka sare moja, huku mara ya mwisho kwa timu hiyo kushinda ni ushindi wa mabao 4-3, dhidi ya KMC FC, Mei 14, 2026.
Matokeo hayo yanaifanya Mbeya City kuendelea kushika nafasi ya 14 na pointi 25, baada ya kushinda mechi sita, sare saba na kupoteza 13, huku Mtibwa ikiwa ya 12 na pointi 27, ikishinda sita, sare tisa na kupoteza 11, kati ya 26, iliyocheza.