Simba Arachuga: Al Ahly anakufa mapema tu

Muktasari:

  • Thabity Ostaz ni katibu wa tawi la Simba Mkoa wa Arusha anasema hawana wasiwasi na mchezo huo kwani tayari wameshajua udhaifu wa mpinzani wao hivyo waalimu wamefanyia kazi hilo kuhakiksha timu yao inashinda.

Arusha. Kwa Mkapa hatoki mtu, ni kauli ya mashabiki wa Simba jijini Arusha ambao wametamba timu yao itaichapa Al Ahly katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Ijumaa hii, Machi 29, 2024.

Mchezo huo utaanza kuanzia saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ambapo mashabiki wa Arusha wanaondoka leo usiku kwenda kuipa sapoti timu yao ikiisaka nusu fainali ya kwanza ya michuano hiyo katika mfumo wa sasa.

Thabity Ostaz, katibu wa tawi la Simba Mkoa wa Arusha, anasema hawana wasiwasi na mchezo huo kwani tayari wameshajua udhaifu wa mpinzani wao hivyo waalimu wamefanyia kazi kuhakiksha timu yao inashinda.

Amesema wanatambua wanakwenda kucheza na timu bora iliyo namba moja Afrika ambayo ina historia kubwa hivyo wamejiandaa na wanaitaka nusu fainali na baada ya kukutana nayo mara kadhaa na safari hii siyo kinyonge, watafanya kitu.

“Wameyakanyaga tunaenda kuwafunga kwa idadi kubwa ya magoli na kuwashangaza wengi kwani hapa ushindi ni lazima tena wa kishindo ili kusonga mbele,” amesema Thabity.

Ameweka wazi kuwa msafara wa mashabiki utaondoka usiku ukiwa na zaidi wa watu 150 kwani lazima wakajaze uwanja na kuonyesha nguvu moja ili kuisapoti timu na kuhakikisha wanafanikisha jambo lao.

“Jana tulikwenda katika kituo cha watoto yatima cha Rescue kipo Kimandolu kwa Shabani lengo ilikuwa ni kuomba dua na watoto pamoja na kufuturu pamoja nao, walituombea dua na tulitoa sadaka hiyo kwa ajili ya mechi yetu,” ameongeza.

Jenipher Raphael anasema wamekuwa wakiingia kwenye hatua hii mara kwa mara na wachezaji wengi wapo wale ambao wanacheza hizi mechi hivyo hana wasiwasi hata kidogo na mchezo huo.

“Kikosi ni kizuri kufika hatua kama hii inaakisi kwamba sisi ni miongoni mwa timu nane bora Afrika, sina shaka na kikosi wala benchi la ufundi,” anasema.

Kwa upande wa Latifa Khamisi anatumia fursa hiyo kuwaomba wachezaji kutambua kwamba wamebeba mioyo ya Watanzania zaidi ya milioni 60 hivyo wanatakiwa kupambana na kupata ushindi.

“Bao chache sana ni mbili ukizingatia tuna mtu kama Zimbwe Jr, Chama, Kapombe ni wachezaji ambao ni waandamizi na wanajua kabisa wana Simba tunataka nini,” amesema Latifa.