Siku 10 za hatari zaibua hofu Yanga

Muktasari:
Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, wataanza kwa kucheza na Bejaia kesho Jumamosi na siku nne baadaye watacheza na Azam katika mchezo wa Ngao ya Hisani kabla ya kusafiri kwenda Kongo ambako siku sita baadaye watavaana na wababe hao wa Lubumbashi.
MABINGWA wa soka nchini, Yanga kesho Jumamosi watashuka Uwanja wa Taifa kuvaana na Mo Bejaia ya Algeria katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini hofu imetanda katika klabuni hiyo kutokana na ratiba ngumu inayowakabili.
Yanga ipo katika hofu, inakabiliwa na ratiba ngumu ndani ya siku 10 zijazo ambapo itacheza na michezo miwili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bejaia na TP Mazembe ya DR Kongo na kisha kucheza mchezo wa Ngao ya Hisani dhidi ya matajiri wa Ligi Kuu Bara, Azam.
Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, wataanza kwa kucheza na Bejaia kesho Jumamosi na siku nne baadaye watacheza na Azam katika mchezo wa Ngao ya Hisani kabla ya kusafiri kwenda Kongo ambako siku sita baadaye watavaana na wababe hao wa Lubumbashi.
Kocha wa Yanga, Hans Pluijm alisema kikosi chake kimefanya maandalizi yote muhimu hivyo hana wasiwasi kuwa wanaweza kufanya vizuri katika michezo hiyo.
“Tunafahamu uzito wa michezo hiyo, timu zote zimejiandaa vizuri lakini nasi hatuko nyuma, tuna maandalizi mazuri pia,” alisema kocha huyo Mholanzi.
Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima alisema ratiba hiyo ni ngumu kwao ila kwa kuwa hakuna namna ya kuipangua ni lazima wapambane na kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika michezo hiyo.
“Sisi ni binadamu kama binadamu wengine, tumetoka katika mashindano na tunaunga kwenda kwenye mashindano mengine, kuna kuchoka pia ila ni lazima tupambane kuhakikisha tunakuwa na matokeo mazuri,” alisema Niyonzima.
Naye beki wa kushoto wa Yanga, Oscar Joshua alisema timu yao iko tayari kwa mapambano katika michezo hiyo na wanafahamu wanahitaji kitu gani hivyo watajitahidi kupambana kuhakikisha wanakipata.