Sikia mingo ya kocha Bizimungu

KOCHA, Ally Bizimungu, anayekinoa kikosi cha Mwadui FC, amefunguka kwamba ametulia kwanza kuhusu usajili wake wa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara mpaka apate uhakika wa wachezaji atakaobaki nao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mrundi huyo alisema kuna wachezaji ambao anajua wanaweza kuondoka baada ya kuhusishwa na klabu nyingine, hivyo anasubiri kujua kama wataondoka kweli au la.

“Nataka kwanza nijue hatma yao ili niwe na uhakika wa wapi pa kuanzia, cha muhimu itakuwa ni kutafuta watu sahihi ambao watakuja kuziba mapengo,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuna maeneo yanahitaji kuboreshwa na ameyataja kuwa ni beki ya kushoto, ushambuliaji na wingi ya kulia na amesema atayaboresha kwa kusajili wanaotoka timu za ligi kuu.

“Nataka kuongeza wachezaji wa nafasi hizo ambao watakuwa na uwezo wa kucheza kwa kiwango cha juu katika mechi mfululizo, msimu uliopita tulikuwa tukipata taabu maeneo hayo,” alisema.

Bizimungu alifunguka zaidi kwamba ameanza harakati za usajili baada ya kufikia sehemu nzuri ya mazungumzo katika kuongeza mkataba wake na mabosi wachimba madini hao.