Sikia hii! Manara aitaka kombaini ya Barca, Man City

Muktasari:

  • Manara asema anajiamini kusema hivyo kwa maana viungozi wamejipanga na wamewaweka wachezaji wao katika saikolojia nzuri

OFISA habari wa klabu ya Simba, Haji Manara baada ya timu yake kushinda bao 1-0, katika mechi dhidi ya Al Ahly ametamba hata kama wakija FC Barcelona, Real Madrid na Man City katika uwanja wa Taifa watawafunga tu.

Manara alisema si kama zije hizo timu peke yao ikiwezekana waunganishe kombaini moja ambayo watawachagua wachezaji bora tupo lakini wakija hapa kwetu uwanja wa Taifa tutakuwa na uwezo wa kuwafunga kama kawaida.

Alisema anajiamini kusema hivyo kwa maana viungozi wamejipanga na wamewaweka wachezaji wao katika saikolojia nzuri ambayo wamewaeleza kuwa mechi yoyote ya kimataifa msimu huu ambayo watacheza nyumbani wanatakiwa kupata ushindi.

"Yaani siku moja kabla ya mechi na Al Ahly wachezaji wa timu yetu waliniambia Manara wewe nenda kapumzike tu, sisi kwetu tutapambana na kuhakikisha ushindi unapatikana na hiyo yote walisema kutokana na tulivyowajenga kiakili," alisema.

"Kubwa tumepata ushindi katika mechi hiyo imeshapita na akili yetu ni kupata pointi tatu nyingine katika mchezo ambao tutacheza hapa nyumbani ili kuona mwisho wa michezo hii ya makundi tunakuwa na uhakika wa pointi tisa ambazo tumepata nyumbani.

"Tumemaliza mechi na Al Ahly inayofata dhidi ya watani zetu Yanga kwa sasa siwezi kueleza lolote lakini muda utakapofika kila kitu nitakiweka wazi kama nilivyofanya katika mechi hizi za Kimataifa," alisema Manara.