Shime atoswa Serengeti Boys

Muktasari:
Oscar Milambo pamoja na Peter Manyika huku Sebastian Mkoma yeye akiwa na jukumu la kuwa kocha mkuu wa timu zote za taifa za wanawake.
Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeachana rasmi na aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya vijana wenye umri wa miaka 17 'Serengeti Boys', Bakari Shime na nafasi yake kuchukuliwa na Kim Poulsen.
Uamuzi huo umewekwa hadharani leo wakati wa kutangaza kikosi cha wachezaji 50 wa timu ya taifa ya wanaume ya vijana wenye umri usiozidi miaka 20 'Ngorongoro Heroes', watakaoingia kambini Jumapili hii kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Niger mwaka 2019.
"TFF inapenda kuutangazia umma kwamba kuanzia sasa, Kim Poulsen ndiye atakuwa kocha mkuu wa timu zetu zote za taifa za vijana kwa wanaume ambapo atakuwa akisaidiwa na Oscar Milambo pamoja na Peter Manyika huku Sebastian Mkoma yeye akiwa na jukumu la kuwa kocha mkuu wa timu zote za taifa za wanawake.
Kwa timu ya taifa ya wanaume 'Taifa Stars', itaendelea kuwa chini ya kocha Salum Mayanga ambaye atasaidiana na Fulgence Novatus," alisema ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas.
Kauli hiyo inaashiria kuwa TFF imemuondoa Shime ambaye alikuwa kocha mkuu na kumpa nafasi hiyo Poulsen ambaye alikuwa ni mshauri wa ufundi wa timu za taifa za vijana za soka za wanaume.
Wakati huohuo, Poulsen ameita wachezaji 50 wa Ngorongoro Heroes ambao watakaa kambini kwa wiki mbili jijini, ambapo kati yao 23 watakuwa nyota waliokuwemo kwenye kikosi cha Serengeti Boys kilichoshiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana zilizofanyika Gabon mwaka huu.
"Baada ya kambi hiyo ya wiki mbili, kutakuwa na mchujo ambapo tutapunguza wachezaji 20 ili wabakie 30 ambao tutaendelea nao kwenye programu zetu.
Naamini kupitia wachezaji hawa tuliowaita, tutafanikiwa kutengeneza timu bora yenye ushindani ambayo itawafanya Watanzania watembee kifua mbele," alisema Poulsen.
Miongoni mwa wachezaji walioitwa ni kipa wa Yanga, Ramadhan Kabwili pamoja na mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Riffat Khamis.