Shikalo awatibulia Kagere, kahata

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Shikalo alisema hesabu zake kubwa katika kutua kwake Yanga sasa ni kuhakikisha anaisaidia klabu hiyo kuchukua taji la Ligi Kuu Bara na kufika mbali kwa timu hiyo katika kampeni ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


HUKO Jangwani kwa sasa kila kitu kipo freshi, kwani mabosi wa klabu hiyo waliamua kutuma vigogo wawili Kigali, Rwanda ili kumaliza usajili Farouk Shikalo na fasta kipa huyo Mkenya akaamua kuwatibulia nyota wa Simba, Meddie Kagere na Francis Kahata.

Shikalo aliye na Bandari Kenya kwenye michuano ya Kombe la Kagame, alizuiwa kuja Tanzania kuungana na nyota wenzake wa Yanga kwa sababu mabosi wake kutibuliwa na kile kilichofanywa na klabu ya Jangwani iliyomsainisha mkataba akiwa timu ya taifa.

Kipa huyo namba mbili alikuwa Cairo, Misri na timu hiyo ya taifa ya Kenya, Harambee Stars kwa ajili ya michuano ya Fainali za Afcon 2019, walipopangwa Kundi C pamoja na Tanzania, Senegal na Algeria na Yanga ilimuibukia huko na kumsainisha mkataba.

Kitendo hicho kiliwatibua mabosi wake na kuongeza dau tofauti na lile waliloweka awali wakati Yanga ilipowafuata, ndipo vigogo hao wawili wakatumwa kwenda kutuliza mambo na kipa huyo akalidokeza Mwanaspoti kuwa kila kitu kwa sasa kipo sawa.

Vigogo walioenda huko ni pamoja na Makamu Mwenyekiti Fradrick Mwakalebela na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Majid Seleman kwa lengo la kumalizana na klabu hiyo juu ya uhamisho huo na kila kitu kinaelezwa kipo poa na Shikalo akaanza tambo zake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Shikalo alisema hesabu zake kubwa katika kutua kwake Yanga sasa ni kuhakikisha anaisaidia klabu hiyo kuchukua taji la Ligi Kuu Bara na kufika mbali kwa timu hiyo katika kampeni ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Shikalo alisema anatambua kikwazo kitakuwa ni watani wao Simba, ambao wana straika Meddie Kagere na kiungo mpya Francis Kahata lakini ameshajua dawa yao.

“Huko Ligi Kuu mnaita Tanzania Premier League sio? Hilo ni lengo langu la kwanza kuhakikisha tunalichukua, lakini kama tutafika mbali Ligi ya Mabingwa pia ni sehemu ya malengo yangu, ingawa natambua tunatakiwa kuweka nguvu kubwa.

,“Najua hapo kuna Simba ambao ni timu pinzani kubwa kwa Yanga, huyo Kagere (Meddie) namjua na ananijua vizuri pia rafiki yangu Kahata (Francis) ameniambia amejiunga nao ni wachezaji wazuri, lakini dawa yao naijua kitambo,” aliongeza Shikalo.

Kipa huyo Bora wa Ligi Kuu Kenya (KPL) alisema amemuona beki mkongwe wa Yanga Kelvin Yondani, kule Misri lakini pia amekuwa akiangalia mikanda ya video ya beki mpya Mghana Lamine Moro na kugundua kwa makali ya mabeki hao Kagere wala Kahata hawawezi kuwa tatizo.

Mbali na Yondani Yanga imembakisha beki Andrew Vincent ‘Dante’ lakini ikawaongeza Moro, Ally Sonso, Ali Ali, Mrundi Mustapha Seleman na Muharami Issa Salum katika ukuta wao wa msimu ujao.

“Yondani nilikuwa naye Misri tulipokutana na Kenya na Tanzania nimemfanyia tathmini ni beki mzuri sana, pia kuna huyo Mghana amesajiliwa (Lamine) nimeangalia video zake nimejiridhisha kwamba tutakuwa na mabeki wazuri hakuna wa kututisha.”

BANDARI MAMBO SAFI

“Uongozi wa Bandari nimekutana nao na wameniambia Yanga walikuja hapa Rwanda na wamekutana nao na nijiandae kuhamia Tanzania, kwa sasa namalizia hizi mechi za Cecafa na baada ya hapo nitarudi Kenya nyumbani unajua sijarejea tangu nimetoka Misri, ila nikitoka hapo naja huko kuungana na Yanga,” alifafanua Shikalo.