Shaffih Dauda afungiwa miaka mitano, mwingine maisha

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kamati yake ya maadili imewafungia wanafamilia wake wawili Shaffih Dauda na Hawaiju Gantala vifungo vikali tofauti.
Taarifa iliyotolewa na TFF saa chache zilizopita imesema kupitia kikao cha Februari 14 na 15 ikisikiliza mashauri hayo mawili tofauti kamati imemtia hatiani Dauda kwa kumfungia kifungo cha miaka mitano na faini ya sh 6 milioni.
Kamati imemtia hatiani Dauda kufuatia chapisho lake kupitia mtandao wa Kijamii wa Instagram kinyume cha 73(4)(a) na 75(5) vya kanuni za maadili za TFF toleo la 2021 pia kwa kukiuka kifungu cha 3(1) cha kanuni za utii za TFF toleo la 2021.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Dauda ambaye ni mjumbe wa Mkutano wa Mkutano Mkuu wa TFF alikiri kuchapisha taarifa hiyo ya Februari 8,2022 lakini akadai akaunti hiyo inaendeshwa na watu wanne tofauti.
Aidha Dauda ameeleza kwamba alishindwa kuihariri taarifa hiyo kwa kuwa alikuwa safarini kutoka Cameroon akirejea jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa Gantala ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu ya Biashara ya Mara,TFF ilimlalamikia kwa kosa la kupeleka masuala ya michezo mahakama za kawaida.
Kosa hilo ni kushindwa kutii ibara ya 59(2) ya Katiba ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na ibara ya 66 ya katiba ya TFF toleo la 2019 kifungu cha 6(1)(a) cha kanuni za maadili za TFF toleo la 2021.
Imeelezwa mlalamikiwa kufuatia kufungua kesi Mahakama ya Wilaya ya Musoma akipinga uchaguzi wa klabu ya Biashara United kuendelea.
Kwa kosa hilo Gantala amefungiwa maisha kujihusisha na soka ndani na nje ya nchi adhabu ikitolewa kwa mujibu wa kifungu cha 6(1),(h),73(3)(c) vya kanuni za maadili za TFF toleo la 2021 na ibara ya 65(2),(f) ya katiba ya TFF toleo la 2019.