Kennedy Musonda atua Israel

Muktasari:
- Jana, Musonda aliwaaga Wananchi ambao amewatumikia kwa miaka miwili na nusu na kuwafungia mabao 34, akitoa asisti 13 ambapo ametwaa mataji matatu ya ligi na FA matatu na ngao za jamii mbili.
SIKU moja baada ya kuwaaga mashabiki wa Yanga baada ya kumaliza mkataba, mshambuliaji Kennedy Musonda amejiunga na Hapoel Ramat Gan inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Israel maarufu kama Liga Leumit.
Jana, Musonda aliwaaga Wananchi ambao amewatumikia kwa miaka miwili na nusu na kuwafungia mabao 34, akitoa asisti 13 ambapo ametwaa mataji matatu ya ligi na FA matatu na ngao za jamii mbili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Musonda amesema amemaliza maisha Tanzania akiwa na mafanikio sasa anakwenda kujaribu maisha Israel ambako ameahidi kuwa anatafuta rekodi nyingine.
“Haijawa rahisi kuhitimisha maisha Yangu ndani ya Yanga licha ya panda shuka, lakini nafurahi nimefanikiwa kutwaa mataji na nimeacha kitu cha kuzungumzwa ndani ya timu hiyo sasa ni wakati wangu kwenda sehemu nyingine,” amesema na kuongeza:
“Ni kweli naenda Israel suala la mkataba wa muda gani nitakufahamisha sio sasa kikubwa ni kwamba nimeshapata timu mpya na nitakuwa Israel msimu ujao.”
Nyota huyo ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Zambia, ameiambia Mwanaspoti kuwa safari moja huanzisha nyingine alipofikia Yanga hakuwa na matarajio makubwa lakini amefanikiwa hivyo anaamini kuwa aendapo pia atafanya makubwa.