Serikali kuboresha uwanja wa Sokoine Mbeya

Muktasari:
- Sokoine ni miongoni mwa viwanja vikubwa nchini ukikadiriwa kubeba watazamaji 25,000 hivyo maboresho yake yatasaidia mashabiki na timu za Mkoa huo kuwa kupata uhondo wa soka.
Mbeya. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema uwanja wa Sokoine ni miongoni mwa viwanja vitakavyofanyiwa maboresho kupitia mfuko wa michezo wa Baraza la michezo nchini (BMT).
Akizungumza jijini hapa leo Alhamisi, Agosti 19 wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Mbeya Super Cup, Bashungwa amesema Sokoine itakuwa miongoni mwa viwanja vitakavyofanyiwa maboresho.
Amesema Mkoa wa Mbeya umekuwa na historia kubwa katika suala la michezo kwa kuwa na timu nyingi kila madaraja hivyo katika kurejesha heshima yake kama miaka ya nyuma lazima iwe na miundombinu iliyo bora.
"Nimefurahishwa na mipango hii ya kiubunifu kwa Mkuu wa Mkoa huu kwa kuanzisha mashindano haya, kupitia mfuko wa michezo wa BMT katika zile asilimia 18 za VAT zilizookolewa zitaelekezwa katika kuboresha viwanja na Sokoine itafanyiwa maboresho" amesema Bashungwa.
Amesema kwa sasa kamati iliyopewa jukumu kuandaa mashindano ya Taifa Cup ipo katika hatua za mwisho kutangaza lini michuano hiyo kuanza, huku akiwapongeza Mbeya kwa kuanza mapema maandalizi.
"Tumekamilisha mpango mkakati wa kitaifa wa maendeleo ya michezo nchini, tumerudisha Taifa Cup ambayo itatangazwa hivi karibuni itatangazwa kuanza kwake, niwapongeze Mbeya kwa maandalizi ya mapema" amesema Bashungwa.
Naye Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera amesema lengo la mashindano hayo ni kupata timu ya Mkoa ambayo itashiriki michuano ya Taifa Cup, kukuza biashara zinazohusiana na zisizohusiana na michezo na kuleta burudani kwa wakazi wa Mbeya.
"Pamoja na malengo mengine, lakini tunakusudia kupata timu ya Mkoa itakayoshiriki mashindano mengine kama Taifa Cup, tumejipanga kuhakikisha Mbeya inakuwa mbele katika michezo nchini" amesema Homera.
Naye Majaliwa Manyima mdau wa soka jijini hapa, amesema bado uwanja wa Sokoine una mapungufu mengi haswa sehemu ya majukwaa pamoja na mitaro kutokuwa katika hali nzuri.
"Kama Waziri alivyoahidi iwapo watatekeleza itakuwa vyema kwa sababu huu uwanja ni kivutio kwa Mkoa wetu, lakini hauna majukwaa mazuri na mitaro yake haina afya kwa mashabiki" amesema Manyima.
UYOLE WARRIORS, MBEYA PEAK ZATAKATA
Timu za Uyole Warriors na Mbeya Peak zimeanza kwa kishindo michuano ya Mbeya Super Cup baada ya kugawa dozi kwa wapinzani.
Mashindano hayo yanashirikisha timu nane kutoka Halmashauri saba za Mkoa huo na bingwa ataondoka na kitita cha Sh 5 milioni kutoka kwa muandaaji, Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera.
Katika mechi za ufunguzi wa Ligi hiyo zilizopigwa katika dimba la Sokoine, mchezo wa saa 8 mchana Mbeya Peak ilichapa Chunya mabao 2-1, huku mashabiki wakifurahia burudani kutoka kwa timu hizo.
Chunya ndio walitangulia kupata bao dakika ya 39 kupitia kwa Fascad Mengo lakini Mbeya Peak waliweza kisawazisha kupitia kwa Baraka Mwalubunja dakika ya 44.
Kipindi cha pili kila timu iliingia uwanjani kusaka bao la ushindi, ambapo pande zote zilitengeneza mashambulizi lakini Juntu Juntu aliweza kuifungia bao la pili Mbeya Peak na kuipa ushindi wa kwanza.
Katika mchezo mwingine uliopigwa majira ya saa 10 jioni, Uyole Worriors waliifanyia mbaya Busokelo kwa kuwakandika mabao 2-1 shukrani kwa kazi nzuri ya Oscar Adam na Dagiri Mnyama walioipa ushindi timu yao, huku Baraka Mwalugoja akiifungia bao la kujifariji Busokelo.
Kocha wa Chunya, Emanuel Paul amesema licha ya kupoteza mechi hiyo, lakini bado wana matumaini ya kuweza kujitetea katika mechi zilizobaki na kufikia malengo.
"Ni kweli tumezidiwa na wapinzani kwa sababu tulipambana na nafasi tukapata ila hatukuweza kuzitumia vyema, tunaenda kusahihisha makosa na kurejea upya"amesema Paul.